03. Hapa ndipo Mtume aliingia kwenye Ka´bah

al-Bukhaariy amepokea kwamba Ibn ´Abbaas amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoona picha ndani ya Nyumba alikataa kuingia mpaka zilipofutwa. Humo aliona picha ya Ibraahiym na Ismaa´iyl (Swalla Allaahu ´alayhimaa wa sallam) mikononi mwao kuna mishale ya bahati nasibu akasema: “Allaah awalaani! Naapa kwa Allaah! Hawakuwahi  kamwe kutumia mishale ya bahati nasibu.”[1]

Abu Daawuud amepokea kuwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja kwa Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambapo akakuta pazia mlangoni na hivyo hakuingia  ndani. Ni mara chache alikuwa akiingia isipokuwa ataanza kwake. Pindi ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alipomuona amehuzunika akamuuliza: ”Una nini?” Akasema: ”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekuja kwangu lakini hakuingia ndani.” ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) akamwendea na kumwambia: ”Ee Mtume wa Allaah! Hakika Faatwimah amehuzunika kwamba umemwendea lakini hukuingia ndani.” Akasema: “Nina nini mimi na dunia? Nina nini mimi na michoro?” ´Aliy akarudi kwa Faatwimah na akamweleza aliyoyasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Akasema: ”Muulize Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nini anachoniamrisha kuyafanya?” Akasema: ”Mwambie ayaagize kwa kabila fulani.”[2]

Kutokana na hayo haiwi Hadiyth hii wala Hadiyth ya Safiynah iliyotangulia miongoni mwa Hadiyth zinazohusu kutengeneza picha, bali ni katika Hadiyth zinazohusu mapazia na mapambo. Baadhi ya waliopokea Hadiyth hizi wameziingiza katika mlango wa kutengeneza picha, na wengine wameziingiza katika mlango wa mapazia.

Abu Daawuud amepokea  kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa), ambaye ameeleza:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamuru ´Umar bin al-Khatwaab (Radhiya Allaahu ´anh) wakati wa ufunguzi wa Makkah – ambaye alikuwa Batwhaa´ – aende Ka´bah na afute kila picha iliyokuwemo humo. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuingia humo mpaka zilipofutwa picha zote zilizokuwemo ndani yake.”[3]

Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaaiy wamepokea kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesimulia kuwa Maymuunah – mkewe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – alimweleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Jibriyl aliniahidi kukutana nami usiku huu, lakini hakukutana nami. Alipokutana naye, Jibriyl akasema: ”Hakika sisi hatuingii ndani ya nyumba ambayo ndani yake kuna mbwa wala picha.”[4]

Hadiyth katika mlango huu ni nyingi. Lengo hapa ni kutoa dalili kwa kile alichouliza muulizaji. Kile nilichotaja mpaka hapa kinatosha. Na hata kama kusingekuwa na nyingine isipokuwa Hadiyth zinazowasema vibaya na kuwalaani watengeneza picha pamoja na kuwasimanga wale wanaojaribu kuumba kama anavyoumba Allaah (Ta´ala) zingetosha.

[1] al-Bukhaariy (3352).

[2] Abu Daawuud (4149). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (4149).

[3] Abu Daawuud (4156). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (4156).

[4] Muslim (2105), Abu Daawuud (4157) na an-Nasaa’iy (4283).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin ´Aliy ash-Shawkaaniy (afk. 1250)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm-ut-Taswwiyr, uk. 22-26
  • Imechapishwa: 06/05/2026