03. Hadiyth kuhusu mwanamke kuonyesha nusu ya mkono wake

Jariyr amepokea kupitia kwa Qataadah ambaye amesema:

”Nimefikiwa na khabari kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho kuonyesha mkono wake isipokuwa mpaka hapa” na akashika nusu ya mkono.”

Cheni hii ya wapokezi imekatika. Baada ya hapo akapokea mfano wake kutoka kwa Ibn Jurayj aliyesimulia kuwa ´Aaishah amesema:

”Nilitoka kumwendea mpwa wangu ´Abdullaah bin at-Twufayl hali ya kuwa nimejipamba. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akachukizwa na hilo na akasema: ”Wakati mwanamke anapobaleghe basi si halali kwake kuonyesha isipokuwa tu uso wake na hiki” na akashika nusu ya mkono wake.”

Hadiyth ni dhaifu na inapingana na Hadiyth zilizo Swahiyh. Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu na inaenda kinyume na Hadiyth yenye nguvu zaidi, nayo ni ile inayokuja iliyopokelewa na Abu Daawuud kutoka kwa ´Aaishah. Yule ambaye ana utambuzi juu ya elimu hii tukufu haweki shaka ya kwamba ndio yenye nguvu zaidi. Kwa sababu inatiliwa nguvu na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambayo ni ile Hadiyth inayokuja ya Asmaa´ pamoja na matendo ya Maswahabah wa kike. Tofauti na Hadiyth hii. Haina mapokezi wala matendo yanayoitia nguvu. Kwa hiyo ni dhaifu na yenye kupingana na Hadiyth zilizo Swahiyh (Munkar).

Katika Hadiyth ya Ibn Jurayj kuna karipio jengine ambalo ni kubwa zaidi kuliko lile lililotangulia, nalo ni kule kwenda kinyume na Qur-aan. Hadiyth inamkemea ´Aaishah kutoka kwenda kwa mpwa wake ´Abdullaah bin at-Twufayl hali ya kuwa ni mwenye kujipamba. Ilihali Allaah (´Azza wa Jall) anasema:

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ

“Na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, baba zao, baba za waume wao, wana wao wa kiume, wana wa kiume wa waume zao, kaka zao, wana wa kiume wa kaka zao, wana wa kiume wa dada zao… “ (24:31)

Hapa kuna dalili ya wazi kufaa kwa mwanamke kuonyesha mapambo yake mbele ya mtoto wa kaka yake. Kwa hivyo Hadiyth ni Munkar kwa mtazamo huu pia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 41-42
  • Imechapishwa: 30/08/2023