2 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesimama [kuswali] usiku wa Qadar kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[1]

Kuna maafikiano juu yake.

Hadiyth inafahamisha juu ya fadhilah za usiku wa Qadar na kisimamo chake na kwamba ambaye atasimama hali ya kumwamini Allaah, akiamini zile thawabu alizowaandalia wale wasimamaji na akitaraji ujira na thawabu, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Nao ni usiku mtukufu ambao Allaah (Ta´ala) ameutukuza na akaufanya kuwa bora kuliko miezi elfu inapokuja katika baraka zake na matendo mema ndani yake. Ni usiku bora kuliko miezi elfu. Ni takriban miaka themanini na tatu na miezi minne.

[1] al-Bukhaariy (04/225) na Muslim (957).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 62
  • Imechapishwa: 26/02/2023