03. Dalili ya pili juu ya kufaradhishwa kufunga Ramadhaan

2 – Imethibiti katika ”as-Swahiyh” ya Muslim ya kuwa kuna mbedui mmoja ambaye alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nywele zikiwa timtim akasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Nieleze ni nini ambacho Allaah amenifaradhishia katika swalah?” Akajibu: “Swalah vipindi vitano isipokuwa kama utapenda kujitolea kitu.” Akasema: “Nieleze ni nini ambacho Allaah amenifaradhishia katika swawm?” Akajibu: “Swawm ya Ramadhaan isipokuwa kama utapenda kujitolea kitu.” Akasema: “Nieleze ni nini ambacho Allaah amenifaradhishia katika zakaah?” Akajibu: “Mtume wa Allaah akamweleza nembo za Uislamu.” Akasema: “Naapa kwa Yule ambaye amekuheshimisha; sintojitolea na wala sintopunguza chochote katika yale ambayo Allaah amefaradhisha.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Amefaulu akiwa mkweli au ataingia Peponi akiwa mkweli.”

Katika Hadiyth hii kuna dalili ya kwamba ambaye atatekeleza mambo ya wajibu na ya faradhi na pia kujiepusha na mambo ya haramu, basi amefaulu na pia ni miongoni mwa watu wa Peponi. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Amefaulu akiwa mkweli au ataingia Peponi akiwa mkweli.”

Aliyasema hayo baada ya kusema kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Sintojitolea na wala sintopunguza chochote katika yale ambayo Allaah amefaradhisha.”[1]

Hawa ndio wale watu wa kati na kati na ndio wema. Iwapo mbali na hivo watajitolea kutekeleza ´ibaadah zinazopendeza – swalah zinazopendeza, swawm zinazopendeza, hajj inayopendeza, jihaad na mengineyo –  basi anakuwa miongoni mwa waliotangulia ambao wamekurubishwa. Hao ndio wale wenye ngazi za juu kabisa. Akifanya upungu katika baadhi ya mambo ya wajibu au akaacha baadhi yake au akafanya baadhi ya mambo ya haramu, basi ni mwenye kijidhulumu nafsi yake. Mtu huyo pia ni miongoni mwa watu wa Peponi ingawa kabla ya hapo anaweza kufikwa na hali nzito au adhabu ndani ya kaburi au Motoni.

Watu sampuli hii tatu ndio watu wa Peponi walioteuliwa ambao Allaah amewarithisha Kitabu. Allaah (Ta´ala) amesema:

ثُمَّ أَوْرَثْنَا الْكِتَابَ الَّذِينَ اصْطَفَيْنَا مِنْ عِبَادِنَا ۖ فَمِنْهُمْ ظَالِمٌ لِّنَفْسِهِ وَمِنْهُم مُّقْتَصِدٌ وَمِنْهُمْ سَابِقٌ بِالْخَيْرَاتِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَضْلُ الْكَبِيرُ جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا يُحَلَّوْنَ فِيهَا مِنْ أَسَاوِرَ مِن ذَهَبٍ وَلُؤْلُؤًا ۖ وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ

“Kisha Tukawarithisha Kitabu wale tuliowateuwa miongoni mwa waja Wetu. Basi miongoni mwao ni aliyedhulumu nafsi yake na miongoni mwao aliyekuwa kati na kati na miongoni mwao aliyetangulia kwa mambo ya kheri kwa idhini ya Allaah – hiyo ndio fadhilah kubwa. Mabustani ya kudumu milele wataziingia, watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu na lulu na mavazi yao humo ni hariri.”[2]

Tunamuomba Allaah Mkarimu kutokana na fadhilah Zake.

[1] al-Bukhaariy (1891) na Muslim (11).

[2] 35:32-33

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ilmaam bishay´ min Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 26/03/2023