02. Uzuri wa mwenye busara huondoa ubaya wa sura yake

1- Mtu akiwa na akili nzuri na sura mbaya unaondoka ubora wa ubaya wa sura yake. Mtu akiwa na sura nzuri na akili pungufu unaondoka uzuri wa sura yake.

2- Mwenye busara haimpasi kuwa na wasiwasi kwa kuwa fakiri. Mwenye busara anaweza kuwa tajiri. Wala mtu asiamini kubaki kwa mali ya tajiri ambaye ni mjinga. Mali ya mwenye busara ni akili yake na matendo yake mema.

3- Maradhi ya mwenye busara ni kiburi, mabalaa mazito na ustawi wenye kupitiliza. Mabalaa yakizidi kuwa mengi, busara zake zinapotea. Akiwa katika hali nzuri, anakuwa ni mwenye jeuri.

4- Ni bora kuwa na rafiki mwenye akili kuliko kuwa na rafiki mjinga.

5- Mu´aawiyah bin Qurrah amesema:

“Kuna watu wenye kuhiji, kufanya ´Umrah, kutoka katika Jihaad, kuswali na kufunga. Hata hivyo siku ya Qiyaamah hawatolipwa isipokuwa kwa kadri ya akili yao.”

6- al-Akkaaf amesema:

“Mwenye busara hadhulumu. Mchaji Allaah hadhulumu.”

7- Kama ambavyo juhudi hazinufaishi pasi na uwafikishwaji na uzuri haunufashi pasi na utamu na kama ambavyo furaha hainufaishi pasi na amani, kadhalika akili hainufaishi pasi na uchaji Allaah wala kumbukumbu pasi na matendo. Kama ambavyo furaha ni yenye kufuata amani na udugu ni wenye kufuata mapenzi, murua wote ni wenye kufuata akili.

8- Mwenye busara haanzi kuzungumza isipokuwa anapoulizwa. Hajadili sana iwapo maneno yake hayakubaliwi. Hakimbilii kujibu isipokuwa baada ya kuthibitisha.

9- Mwenye busara hamdharau yeyote. Anayemdharau mtawala anaharibu dunia yake. Ambaye anawadharau wachaji Allaah anaiangamiza dini yake. Mwenye kuwadharau ndugu zake anapoteza murua wake. Anayemdharau ambaye si msomi anaishi khatarini.

10- Mwenye busara ni yule mwenye kuzitambua kasoro zake mwenyewe. Asiyeona mapungufu yake basi vilevile haoni mazuri ya wengine. Miongoni mwa adhabu mbaya kabisa ni mtu kutoona kasoro zake mwenyewe. Kwa kuwa asiyeona mapungufu yake basi hayaachi pia. Kadhalika mtu hatozingatia mazuri ya wengine endapo hayafahamu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 13/10/2016