1- Sikuhifadhi kitu sahihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu akili.

2- Mtu kupenda tabia njema na kuchukia tabia mbovu si jengine isipokuwa ni akili.

3- Kwa akili mtu anafikia bahati, upweke unakuwa mzuri na inaondosha ufukara. Hakuna mali yoyote iliyo bora kama akili na dini ya yeyote haikamilika isipokuwa mpaka itimie akili yake.

4- Habiyb al-Jallaab amesema:

“Nilimuuliza Ibn-ul-Mubaarak kuhusu kitu bora alichopata mtu. Akasema: “Akili ya kina.” Nikasema: “Asipokuwa nayo?” Akasema: “Adabu nzuri.” Nikasema: “Asipokuwa nayo?” Akasema: “Ndugu mwema mwenye kumshauri.” Nikaseama: “Asipokuwa nae?” Akasema: “Kunyamaza kwa muda mrefu.” Nikasema: “Asipokuwa na hilo?” Akasema: “Kifo cha haraka.””

5- Kuna aina mbili ya akili. Ya kwanza ni ya kimaumbile. Ya pili ni yenye kutoka kwenye Wahy. Ya kimaumbile ni kama ardhi na ya Wahy ni kama maji. Akili ya kimaumbile haiwezi kufanya kitendo cha sawa isipokuwa baada ya kutakasika na Wahy unaoiamsha na kuisalimisha na mambo yenye kughuri.

6- Mwenye busara anatakiwa kuihuisha akili yake zaidi kwa hekima kuliko [anavyoutazama] mwili wake kwa chakula. Lishe ya mwili ni chakula na lishe ya mwenye busara ni hekima. Kama jinsi mwili unakufa pale unapokosa chakula na kinywaji, vivyo hivyo mwenye busara anakufa pindi anapokosa hekima.

7- Kuzunguka ulimwenguni na kuzingatia uumbaji wa Allaah kunaifanya akili ya mtu kuzidi hata kama mali itaisha katika kuzunguka kwake.

8- Akili ndio dawa ya mioyo, kipando cha wenye kujitahidi, shamba la Aakhirah, taji la muumini duniani na silaha kipindi kunapotokea majanga. Mwenye kukosa akili ufalme wake hautomsaidia kuweza kufikia utukufu wala mali yake kuweza kufikia hadhi. Kama ambavyo ujinga ndio ugonjwa mbaya kabisa kadhalika kukosa akili ndio ugonjwa mbaya kabisa.

9- Akili na matamanio ni vitu viwili vilivyo kinyume. Ni wajibu kwa mtu kuisaidia akili yake na kuyaahirisha matamanio yake. Viwili hivyo vinapotatiza basi mtu anatakiwa achague kile kilicho mbali zaidi na matamanio. Pindi mtu anapoyaepuka matamanio yake na kuichunga akili yake, inatengemaa dhamira ya mtu.

10- Mwenye busara hatakiwi kuwa na huzuni. Unyogovu haufaidishi kitu. Kuwa na unyogovu mwingi kunapunguza akili. Mwenye busara hatakiwi vilevile kusikitika. Mahuzuniko hayaondoshi majanga. Mahuzuniko yenye kuendelea yanapunguza akili.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 16-20
  • Imechapishwa: 13/10/2016