02. Uharamu wa kufunga siku 1 au 2 kabla ya Ramadhaan

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Hakika swawm inazo hukumu na adabu za wajibu na zinazopendeza. Miongoni mwa hukumu zake kabla ya kuanza kwake:

1 – Ni haramu kufunga siku moja au mbili kabla ya Ramadhaan. Hapo ni pale ambapo mtu atafanya hivo kwa lengo la kuchukua tahadhari kwa ajili ya Ramadhaan. Lakini ikiwa alikuwa na mazowea ya kufunga na siku yake ikakutana na Ramadhaan – na hakukusudia kuchukua tahadhari kwa ajili ya Ramadhaan – ni sawa akaendelea na funga yake. Mfano wa hilo ni kama ambaye ana mazowea ya kufunga swawm ya alkhamisi na ikakutana na mwisho wa mwezi. Mfano mwingine ni kama ambaye anafunga swawm ya wajibu, kama vile swawm ya nadhiri au swawm ya kulipa deni la Ramadhaan iliyotangulia. Hilo ni kutokana na yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiitangulizie mmoja wenu Ramadhaan kwa kufunga siku moja au siku mbili; isipokuwa ikiwa ni mtu aliyezowea kufunga swawm yake basi afunge siku hiyo.”[1]

Hili ni tamko la al-Bukhaariy. Tamko la Muslim linasema:

“Msiitangulie Ramadhaan kwa kufunga siku moja au mbili; isipokuwa mtu aliyezowea kufunga swawm yake basi aendelee kuifunga.”[2]

Pia kutokana na yale yaliyopokelewa katika Hadiyth ya ´Ammaar bin Yaasir (Radhiya Allaahu ´anh) ilioko kwa al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu hali ya kuashiria kuthibiti kwake na cheni ya wapokezi wake imeungana katika as-Sunan:

“Yeyote mwenye kufunga siku ya shaka, basi hakika amemuasi Abul-Qaasim.”[3]

[1] al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082).

[2] al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082).

[3] al-Bukhaariy (03/27).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 13
  • Imechapishwa: 11/04/2023