02. Qur-aan inakuja kwa haki na tafsiri nzuri zaidi

Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

“Wala hawakujii kwa mfano wowote isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri bora kabisa.”[1]

Yale yote yanayoletwa na watu wa batili, wanayotatiza kwayo katika propaganda zao za kupotosha, kuwaelekeza kwao wengine kwa aina mbalimbali ya batili, kuwachanganya wengine kuhusu yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), yote hayo yanasambaratika na kufichuka kwa yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah na Mtume Wake kwa ibara za wazi zaidi, ubainifu kamilifu zaidi na kwa hoja barabara zinazojaza mioyo na kuisapoti haki. Hilo si kwa jengine isipokuwa ni kwa sababu elimu inachukuliwa kutoka ndani ya Kitabu kitukufu na Sunnah takasifu. Ni elimu yenye kutoka kwa mwingi wa hekima, Mjuzi wa kila kitu. Anazijua hali za waja, anajua matatizo yao, anajua yaliyomo ndani ya nafsi zao katika fikira mbaya au fikira zilizo salama. Vilevile anajua yale yanayoletwa na watu wa batili kwa yale yanayokuja huko mbele katika zama. Yote hayo anayajua (Subhaanah).

Amekiteremsha Kitabu Chake ili kuiweka wazi zaidi haki na kufichua batili, kusimamisha hoja kwa yale waliyolingania kwayo Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam).

Amemtuma Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa uongofu na dini ya haki. Ameteremsha Kitabu Chake kitukufu hali ya kuwa ni chenye kubainisha kila kitu, uongofu na bishara njema kwa kila muislamu.

[1] 25:33

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 09/11/2021