Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Mwisho mwema ni kwa wale wenye kumcha. Swalah na salamu zimwendee Mtume Wake, mbora katika viumbe Wake, mwaminifu zaidi juu ya Wahy Wake; Mtume wetu Muhammad bin ´Abdillaah, kizazi chake, Maswahabah na wale waliofuata njia yao na uongofu wao mpaka siku ya Malipo.

Wa ba´d:

Hapana shaka kwamba elimu ndio funguo ya kheri zote na ndio njia yenye kumfanya mtu akatekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia na akaacha yale aliyomuharamishia. Hakika matendo ni natija ya elimu kwa yule ambaye Allaah amemuwafikisha. Elimu ndio ambayo hutilia nguvu ile azma ya kila kheri. Kwa msemo mwingine ni kwamba hakuna imani, matendo, mapambano wala jihaad isipokuwa kwa elimu. Hiyo ina maana kwamba maneno na vitendo bila elimu havina maana wala manufaa yoyote. Bali mwisho wake unakuwa mbaya. Bali pengine vikapelekea katika uharibifu mkubwa.

Hakika si vyenginevyo Allaah anaabudiwa, kutekeleza haki Yake, kueneza dini  Yake, kupiga vita fikira mbovu, propaganda za kupotosha na harakati zilizopinda kwa elimu yenye manufaa inayochotwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Namna hiyo pia faradhi zinatekelezwa kwa elimu. Allaah anaogopwa kwa elimu. Kupitia elimu ndio kunafichuliwa hakika zilizopo ndani ya Qur-aan na Sunnah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 09/11/2021