Kuswali Sunnah ya Fajr wakati imamu amekwishaanza kuswali Fajr

Swali: Wako wanaoingia na imamu amesimama. Lakini wanajua kuwa imamu anarefusha katika Rak´ah ya kwanza. Hivyo anaswali Rak´ah mbili za Fajr kabla hajajiunga pamoja na imamu. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Hili halijuzu. Kwa sababu Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) inafahamisha kuwa maamuma akiingia akamkuta imamu amekwishaanza swalah, basi apange safu. Katika hali hii asiswali Raatibah ya Fajr wala swalah nyingine. Bali apange safu pamoja na imamu. Imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Kunapokimiwa swalah basi hakuna swalah nyingine isipokuwa ile ya faradhi.”[1]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Ni lazima kwa ambaye ameingia na imamu amekwishasimama basi aswali pamoja na imamu. Acheleweshe Sunnah mpaka baada yaa swalah au baada ya kuchomoza kwa jua. Kuhusu kuiswali na huku imamu anaswali ni jambo lisilojuzu kutokana na Hadiyth iliyotajwa.

[1] Ahmad (9563), Muslim (710) na Abu Daawuud (1266).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/370)
  • Imechapishwa: 08/11/2021