01. ´Aqiydah moja pekee sahihi, nyenginezo zote ni batili

´Allaamah na hoja ya Uislamu Abu Ja´far al-Warraaq at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema Misri:

1 – Huu ni ubainifu wa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa mujibu wa madhehebu ya wanachuoni wa Uislamu Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit al-Kuufiy, Abu Yuusuf bin Ibraahiym al-Answaariy na Abu ´Abdillaah Muhammad bin al-Hasan ash-Shaybaaniy na yale wanayoamini katika misingi ya dini na kumuabudu kwayo Mola wa walimwengu – Allaah awawie radhi.

MAELEZO

Tambua kwamba yale aliyotaja mtunzi (Rahimahu Allaah) katika kitabu hiki sio maalum kwa maimamu hawa waliotajwa peke yao. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wote wana ´Aqiydah moja kwa sababu ni wenye kushikamana na Qur-aan na Sunnah.

Yule mwenye kwenda kinyume nao katika ´Aqiydah yao anakuwa mzushi mpotevu. Hapewi udhuru kwa Ijtihaad yake kwa sababu Ijtihaad ni yenye kukubaliwa katika mambo ya mataga na si katika misingi ya dini. Inapokuja katika misingi ya dini hakutakiwi kuwepo mirengo mbalimbali. ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah pekee ndio ya sahihi. Nyenginezo zote ni batili, hivyo zingatia jambo hilo.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad bin ´Abdil-´Aziyz bin Maaniy´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haashiyah ´alaa al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 15
  • Imechapishwa: 09/11/2021