Waumini wanafurahi kwa kufika kwake furaha kubwa. Yule ambaye ametunukiwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa), akakunjuliwa muda wake wa kueshi na akarefushiwa umri wake ambapo akafika ndani ya mwezi huu mtukufu ni neema kubwa kwa mja. Amempa muda na kurefusha maisha yake ili aweze kushiriki na wengine msimu huu mtukufu na uliobarikiwa. Ni msimu wa matendo mema, imani na kujikurubisha kwa Mwingi wa huruma (Subhaanahu wa Ta´ala).

Imepokelewa katika Sunnah Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa bishara njema Maswahabah zake kwa kufika kwa mwezi huu. Imekuja katika Hadiyth ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwaambia Maswahabah zake:

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan – ni mwezi wenye baraka. Allaah amekufaradhishieni kufunga. Ndani yake milango ya Pepo hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa na mashaytwaan waovu hutiwa pingu. Humo Allaah ana usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu moja. Mwenye kunyimwa kheri zake kwa kweli amenyimwa.”[1]

Umekujieni mwezi wa Ramadhaan maana yake ni kwamba hii ni pongezi kwenu, khabari juu ya jambo kubwa mlilopata. Nalo ni kwamba mwezi wa Ramadhaan umekujieni hali ya kuwa mko katika uzima na afya njema na mnaburudika kwa amani, imani, usalama na Uislamu. Umekujieni mwezi wa Ramadhaan. Inahusiana na msimu mtukufu kwa ajili ya kumwelekea Allaah, kuifanya hesabu nafsi na kumtii Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) na kujitenga mbali na mambo ambayo yameharamishwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa).

[1] Ahmad (7148) na an-Nasaa´iy (2106) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 05-06
  • Imechapishwa: 02/04/2022