02. Namna ilivyo kubwa haki ya mume kwa mke wake

1 – Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِلرِّجَالِ عَلَيْهِنَّ دَرَجَةٌ

“Na wanaume wana daraja zaidi juu yao.”[1]

Ibn Kathiyr amesema:

“Bi maana katika ubora, maumbile, tabia, nafasi, kutii amri, matumizi, kusimamia manufaa na fadhilah duniani na Aakhirah.”[2]

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila nafsi katika wanadamu ni bwana na mwanamme ni bwana wa familia yake na mwanamke ni bwana wa nyumba yake.”[3]

“Lau ningelimwamrisha yeyote kumsujudia mwingine, basi ningelimwamrisha mwanamke kumsujudia mume wake. Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi Mwake mwanamke hazingatiwi kuwa ameketeleza haki ya Mola Wake mpaka atekeleze haki ya mume wake. Lau kama atamtaka nafsi yake [wafanye jimaa] na yeye mwanamke yuko katika kitanda cha kujifungua[4] basi hatomkatalia.”[5]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Haisilihi kwa mtu kumsujudia mtu mwingine. Endapo ingesilihi kwa mtu kumsujudia mtu mwingine, basi ningelimwamrisha mwanamke kumsujudia mume wake kutokana na ukubwa wa haki yake kwake. Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake lau kuanzia miguuni mwake mpaka juu ya kichwa chake kutakuwa na vidonda vinavyopasukapasuka kisha [mume] akamwelekea ambapo [mke] akaviramba kwa ulimi wake bila kuona kinyaa, basi atazingatiwa hajatekeleza haki yake.”[6]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Haki ya mume juu ya mke wake endapo atakuwa na vidonda au pua yake ikawa inatokwa na usaha au damu kisha [mke yule] akavinyonya, atazingatiwa hajatekeleza haki yake.”[7]

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Si haki kwa mwanamke akafunga na mume wake hakusafiri pasi na idhini yake[8] na chochote anachokitoa pasi na amri yake basi na mume atapata nusu yake.”[9]

´Allaamah al-Albaaniy amesema:

“Ikiwa imewajibishwa kwa mwanamke kumtii mume wake katika kukidhi matamanio yake, basi ana uwajibu zaidi kumtii katika mambo ambayo ni muhimu zaidi kuliko jambo hilo [la kukidhi matamanio yake] kama mfano wa kuwalea watoto wao, kutengeneza familia yao na haki nyenginezo ambazo ni za lazima.”[10]

Haafidhw amesema:

“Katika Hadiyth kuna faida kwamba haki ya mume imekokotezwa zaidi kwa mwanamke kuliko ´ibaadah zilizopendekezwa. Kwa sababu haki yake ni ya lazima. Kufanya ´ibaadah za lazima kunatangulizwa kabla ya kufanya ´ibaadah zilizopendekezwa.”[11]

[1] 02:228

[2] Tafsiyr-ul-Qur-aan al-´Adhwiym (01/271).

[3] an-Nasaa´iy katika ”´Amal-ul-Yawm wal-Laylah” na ipo katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (4441).

[4] Maana yake ni kuwahimiza kuwatii waume zao na kwamba haifai kwao kukataa licha ya hali hii. Tusemeje katika hali nyingine?

[5] Ibn Maajah (1853), Ibn Hibbaan (06/186) na Ahmad (04/381). al-Albaaniy amesahihisha isnadi ya Ahmad kwa mujibu wa sharti za Muslim katika ”as-Swahiyhah” (03/202).

[6] Ahmad (03/159) na wengineo. at-Tirmidhiy amefanya cheni ya wapokezi wake kuwa ni nzuri katika “Targhiyb at-Tarhiyb” (03/55) na pia inapatikana katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (7602).

[7] al-Bazzaar (1465 – Kashf) kwa cheni ya wapokezi nzuri na wapokezi wake ni waaminifu wanaotambulika. Hivo pia ndivo alivosema at-Tirmidhiy katika ”at-Targhiyb wat-Tarhiyb” (03/54), Ibn Hibbaan (06/184 – Ihsaan), al-Haakim (02/189) na wengineo. Ipo pia katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´ as-Swaghiyr” (3143).

[8] an-Nawawiy amesema:

”Sababu yake ni kuwa mume ana haki ya kustarehe naye katika siku yoyote. Haki yake juu yake mke ni lazima papohapo. Haki yake haipotei kwa jambo lililopendekezwa wala jambo la lazima lakini linaweza kucheleweshwa.” (Sharh Muslim (07/115).

[9] al-Bukhaariy (09/16 – Fath), Muslim (1026) na wengineo.

[10] Aad-uz-Ziffaaf, uk. 282 chapa ya Maktaba-ul-Islaamiyyah.

[11] al-Fath (09/296).

  • Mhusika: Shaykh Muhammad Shuwmaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 7-11
  • Imechapishwa: 14/09/2022