02. Mlinganizi amfanyie upole anayestahiki upole na kinyume chake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah Akurehemu. 

MAELEZO

Tambua – Ni neno linaloashiria kutilia umuhimu maudhui. Akisema ”tambua” ina maana kwamba jambo ambalo anataka kukwambia ni muhimu. Kwa hiyo neno hili linafahamisha umuhimu wa maudhui ambayo mtu anataka kuanza.

Maana ya ”tambua” ni kitendo cha amri kinachotokana na elimu. Kwa msemo mwingine jifunze. Elimu maana yake ni kukijua kitu juu ya uhalisia wake au kuwa na taswira ya kitu juu ya uhalisia wake. Ama kukijua au kuwa na taswira ya kitu kinyume na uhalisia wake ni ujinga na ndio kinyume cha elimu.

Allaah akurehemu – Hii ni du´aa anamwombea mwanafunzi. Shaykh anawaombea wanafunzi kwamba Allaah awarehemu na awape huruma Yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Hapa kuna mwalimu kumfanyia huruma mwanafunzi na kwamba anaanza kwa maneno mazuri na du´aa njema ili aweze kumwathiri na akubali kutoka kwa mwalimu wake. Ama mwalimu akimwanzia mwanafunzi wake kwa maneno susuwavu au maneno yasiyonasibiana kitendo hicho kinamkimbiza.

Kwa hiyo ni lazima kwa mwalimu, yule anayelingania kwa Allaah na yule anayeamrisha mema na kukataza maovu kufanya upole kwa yule anayemzungumzisha kwa kumuombea du´aa, kumsifia na maneno laini. Mambo haya yako karibu zaidi na kukubaliwa. Kuhusu ambaye ni mkaidi na anayefanya kiburi ana uzungumzishwaji wa aina nyingine. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ ۖ وَقُولُوا آمَنَّا بِالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْنَا وَأُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَـٰهُنَا وَإِلَـٰهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ

“Na wala msibishane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi; isipokuwa wale waliodhulumu katika wao. Na semeni: “Tumeyaamini ambayo yameteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja pekee; nasi Kwake tunajisalimisha.”[1]

Wale waliodhulumu miongoni mwa Ahl-ul-Kitaab, wakafanya ukaidi na kiburi hawazungumzishwi kwa njia nzuri. Bali wanazungumzishwa kwa njia inayowastahiki. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ ۚ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Ee Nabii! Pambana na makafiri na wanafiki na kuwa mkali kwao na makazi yao ni Motoni; na ubaya ulioje mahali pa kuishia.”[2]

Wanafiki hawapigwi vita kwa silaha. Wanapigwa jihaad kwa hoja, maneno na kuwaraddi kwa ukali ili kuwatokomeza na kuwafanya watu wawakimbie mbali. Amesema (Ta´ala) juu yao:

وَقُل لَّهُمْ فِي أَنفُسِهِمْ قَوْلًا بَلِيغًا

“Waambie maneno yatakayowafika kwelikweli.”[3]

Hawa wanazungumzishwa kwa njia maalum. Kwa sababu ni wakaidi na wajeuri na hawaitaki haki. Wanachotaka ni kuwapotosha watu. Watu hawa wanazungumzishwa kwa njia inayowastahiki.

Ama mwanafunzi anayetaka uongofu anazungumzishwa kwa upole, huruma na ulaini. Kwa sababu anataka haki, elimu na faida.

Allaah akurehemu – Amekuombea rehema. Allaah akikurehemu basi unakuwa ni mwenye kufaulu duniani na Aakhirah pindi unapoingia ndani ya rehema za Allaah. Hii ni du´aa kutoka kwa mwanachuoni mtukufu na mtu mwema. Kuna matarajio ya kukubaliwa – Allaah akitaka.

[1] 29:46

[2] 09:73

[3] 04:63

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 11-15
  • Imechapishwa: 18/11/2020