02 – Mawaidha

Wanachuoni wamekubaliana juu ya kwamba Allaah (Ta´ala) hakuteremsha mawaidha na maonyo makubwa zaidi kama utambuzi na elimu. Inahusiana na mwanadamu kutambua kuwa Mola wake (Jalla wa ´Alaa) ni mwenye kumchunga na ni mtambuzi kwa kila kile anachokificha na kukidhihirisha.

Wanachuoni wamepigia mfano wa mawaidha na maonyo haya makuwa. Wanasema:

Tukadirie kuna mfalme jasiri mwenye kumwaga damu na kuua watu hovyo. Nyuma yake kuna katili na upange wake mkononi mwenye kumwaga damu. Pembezoni mwake huyo mfalme kuna wasichana na wakeze. Ni jambo linawezekana kwa yeyote katika walioko pale kufikiria kumshambulia mmoja katika wale wasichana au wakeze ilihali ni mwenye kujua anachokifanya na anamuona? Hapana. Allaah ana sifa za juu zaidi.  Walioko pale wote watakuwa na woga na wenye kunyenyekea. Kikubwa watachokuwa wanataraji ni amani na usalama.

Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote ya kwamba Allaah (´Azza wa Jall) anaona na kutambua zaidi kuliko mfalme huyu. Adhabu Yake vilevile ni kubwa na yenye kuumiza zaidi. Lau watu wa mji wangelijua kuwa mfalme wao anayajua yale yote wanayoyafanya usiku, basi usiku mzima ungalipita hali ya kuwa na khofu na wasingefanya maovu yoyote.

Amebainisha (Ta´ala) hekima ya kuumba viumbe kwa ajili yake, nayo ni kuwajaribu na kuwapa mtihani ni nani kait yao aliye na matendo mema zaidi.

إِنَّا جَعَلْنَا مَا عَلَى الْأَرْضِ زِينَةً لَّهَا لِنَبْلُوَهُمْ أَيُّهُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Hakika Sisi tumefanya vilioko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwajaribu nani miongoni mwao mwenye matendo mema zaidi.”[1]

Amesema mwanzoni mwa Suurah “Huud”:

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Yeye ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita na ‘Arshi Yake ikawa juu ya maji ili akujaribuni nani kati yenu mwenye matendo mema zaidi.”[2]

Hakusema ´ni nani kati yenu mwenye matendo mengi zaidi`. Amesema katika Suurah “al-Mulk”:

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا

“Ambaye Ameumba mauti na uhai ili akujaribuni ni nani kati yenu mwenye matendo mema zaidi.”[3]

Aayah hizi mbili zinabainisha makusudio ya maneno Yake:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Na Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[4]

Pindi ilipokuwa hekima ya viumbe ipo katika majaribio yaliyotajwa, ndipo Jibriyl akataka kuwaonyesha wanadamu wote ni namna gani watapasi kwenye mtihani huo. Alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ihsaan ni kitu gani?”

Ihsaan ndio kile ambacho viumbe wameumbwa kwa ajili yake ili wajaribiwe nayo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akabainisha njia ya ihsaan hii ni mawaidha na maonyo haya makubwa na kusema:

“Ni kumwabudu Allaah kama vile unamuona na ikiwa wewe humuoni basi Yeye anakuona.”[5]

Kwa ajili hiyo ndio maana huwezi kufungua ukurasa wowote katika Qur-aan tukufu, isipokuwa utakuta mawaidha haya makubwa:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖوَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَال ِ قَعِيدٌ مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

“Hakika Tumemuumba mwanadamu na tunajua yale yanayomshawishi nafsi yake na sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo. Pale wanapopokea wapokeaji wawili wanaokaa kuliani na kushotoni. Hatamki kauli yoyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha [kurekodi].”[6]

فَلَنَقُصَّنَّ عَلَيْهِم بِعِلْمٍ ۖ وَمَا كُنَّا غَائِبِينَ

“Kisha Tutawasimulia kwa ujuzi [yote waliyoyatenda] na hatukuwa wenye kukosekana.”[7]

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِيكِتَابٍ مُّبِينٍ

“Hushughuliki katika jambo lolote na wala husomi humo chochote katika Qur-aan na wala hamtendi matendo yoyote isipokuwa Tunakuwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichiki kwa Mola wako chochote cha uzito wa atomu katika ardhi wala mbinguni na hata kidogo kuliko hicho na hata kikubwa zaidi ya hicho isipokuwa kimo katika Kitabu chenye kubainisha.”[8]

أَلَا إِنَّهُمْ يَثْنُونَ صُدُورَهُمْ لِيَسْتَخْفُوا مِنْهُ ۚ أَلَا حِينَ يَسْتَغْشُونَ ثِيَابَهُمْ يَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ ۚ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ

“Tanabahi! Hakika wao wanageuza vifua vyao ili wamfiche Allaah. Tanabahi! Jueni kuwa wanapojigubika nguo zao Yeye anayajua wanayoyafanya siri na wanayoyatangaza. Hakika Yeye ni mjuzi kwa yaliyomo vifuani.”[9]

Mifano kama hii katika Qur-aan ni mingi.

[1] 18:07

[2] 11:07

[3] 67:02

[4] 51:56

[5] al-Bukhaariy (1/18) na Muslim (1/38-39)

[6] 50:16-18

[7] 07:07

[8] 10:61

[9] 11:05

  • Mhusika: Imaam Muhammad Amiyn ash-Shanqiytwiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Islaam diyn al-Kaamil, uk.11-12
  • Imechapishwa: 13/06/2023