Katika kumi hili ndio mwisho wa mwezi. Matendo huzingatiwa ule mwisho wake. Pengine mtu akakutana na ule usiku wa Qadar ilihali ni mwenye kusimama kuswali kwa ajili ya Mola wa walimwengu ambapo akasamehewa madhambi yake yaliyotangulia. Ni lazima kwa muislamu azidishe ´ibaadah ikiwa alianza mwezi wake kwa mapungufu na ajipambe kwa subira juu ya utiifu. Matendo huzingatiwa ule mwisho wake.

Salaf walikuwa wakirefusha swalah ya usiku kutokana na kumuigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). as-Saaib bin Yaziyd amesema:

“´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alimwamrisha Ubayy bin Ka´b na Tamiym ad-Daariy (Radhiya Allaahu ´anhumaa) wawaswalishe watu Rak´ah kumi na moja. Amesema: “Msomaji alikuwa akisoma mamia ya Aayah mpaka tulikuwa tukiegemea juu ya vijiti kutokana  na urefu wa kisimamo. Hatukuwa tukiondoka isipokuwa karibu na wakati wa Fajr.”[1]

Muumini ndani ya Ramadhaan anakusanyikiwa na mapambano aina mbili ya nafsi yake:

1 – Mapambano ya mchana ya kufunga.

2 – Mapambano ya usiku ya kisimamo.

Ambaye nafsi yake ataikusanyia mapambano haya mawili na akayatekelezea haki zake, basi huyo ni miongoni mwa wenye kusubiri ambao watajazwa ujira wao pasi na hesabu.

Ni lazima kwa mtu kuwahimiza familia yake, kuwapa uchangamfu na kuwapendezeshea ´ibaadah na khaswa katika misimu hii mitukufu ambayo hakuna ambaye anazembea kwayo isipokuwa aliyenyimwa. Kuamka ni kitu kimekuwa chepesi katika wakati wa sasa. Lakini kinachotakikana ni kuwaelekeza familia na vijana chipukizi kufaidika na nyakati za usiku. Sambamba na hilo akawatahadharishe kutokamana na porojo. Khatari zaidi kuliko yote hayo ni mtu umpite wakati kipindi ambapo watu wanaswali swalah ya usiku na yeye yuko katika vikao vya haramu na mikusanyiko yenye madhambi. Hiyo ndio khasara. Tunaomba Allaah usalama.

[1] Maalik katika ”al-Muwattwa´” (01/115) na cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh. 

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 60-61
  • Imechapishwa: 25/02/2023