Inapokuja katika makadirio basi Ummah wa Kiiislamu umegawanyika sehemu tatu:

Ya kwanza: Kundi lililothibitisha makadirio kwa kupindukia na wakakataa uwezo na utashi wa mja. Wanasema kuwa mja hana uwezo wala utashi na kwamba ni mwenye kutenzwa nguvu na hana khiyari. Wanamfananisha na mti unaopelekwa na upepo. Hawatofautishi kati ya kitendo anachofanya mja kwa khiyari yake na kitendo kinachomtokea pasi na khiyari yake. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba watu hawa ni wapotevu. Ni jambo linalojulikana fika kidini, kiakili na kidesturi ya kwamba mtu anatofautisha kati ya kitendo cha khiyari na kitendo kisichokuwa cha khiyari.

Ya pili: Kundi lililothibitisha uwezo na utashi wa mja kwa kipindukia. Wamefikia kiasi cha kwamba wanapinga Allaah (Ta´ala) kuwa na utashi, anataka au anaumba kitendo cha mja. Wanadai ya kwamba mja anatenda kivyake. Baadhi yao wamepitiliza na kufikia mpaka kusema ya kwamba Allaah (Ta´ala) hajui yale wanayotenda waja isipokuwa baada wameshayafanya. Hawa pia wamepitiliza hali ya juu katika kuthibitisha uwezo na utashi wa mja.

Ya tatu: Waumini walioamini wakaongozwa na Allaah kwenye haki katika yale mambo watu wametofautiana kwayo. Nao ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Katika hayo wamepita njia ya kati na kati na wameshikamana na dalili za Kishari´ah na za kiakili. Wanasema kuwa matendo ambayo Allaah (Ta´ala) anaumba kwa walimwengu yamegawanyika aina mbili:

Aina ya kwanza: Yale matendo ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anayafanya yapitike kwa viumbe Wake. Hapa hakuna anayeweza kuathiri kitu. Mfano wa matendo haya ni kunyesha mvua, kuota mazao, uhai, kifo, maradhi, afya njema na mambo mengine ambayo yanaonekana katika viumbe vya Allaah (Ta´ala). Hapa hakuna anayeweza kuathiri kitu. Yote yanahusiana tu na utashi wa Allaah (Ta´ala), aliye Mmoja pekee anayedhibiti mambo yote kwa nguvu.

Aina ya pili: Yale matendo yanayofanywa na viumbe wote kwa kutaka kwao. Matendo haya yanapitika kutokamana na kutaka na utashi wa watendaji. Kwa kuwa Allaah (Ta´ala) ameyafanya hayo kwao. Allaah (Ta´ala) amesema:

لِمَن شَاء مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ

“Kwa yule miongoni mwenu anayetaka anyooke.”[1]

مِنكُم مَّن يُرِيدُ الدُّنْيَا وَمِنكُم مَّن يُرِيدُ الْآخِرَةَ

“Miongoni mwenu wako wenye kutaka dunia na miongoni mwenu wako wanaotaka Aakhirah.”[2]

فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ

“Anayetaka aamini na anayetaka akufuru.”[3]

Mtu anaelewa yale anayoyafanya kwa kutaka kwake na yale anayoyafanya kwa kutokutaka kwake na kwa kutenzwa nguvu. Mtu anateremka kwenye ngazi kwa kutaka kwake kutoka juu ya paa na anajua kuwa anafanya hivo kwa khiyari. Lakini endapo ataanguka kutoka juu ya paa anatambua kuwa hakufanya hivo kwa kutaka. Anatambua tofauti kati ya matendo hayo mawili na kujua kuwa kitendo cha kwanza ilikuwa ni kwa kutaka kwake na kitendo cha pili haikuwa kwa kutaka kwake. Watu wote wanayajua haya.

[1] 81:28

[2] 03:152

[3] 18:29

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Qadhwaa’ wal-Qadar, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (5/216-217)
  • Imechapishwa: 25/10/2016