02. Mahimizo ya kuanza kwa Basmalah na Hamdalah katika mambo muhimu

Maneno ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah):

“Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”

Kuanza kwa Basmalah na Hamdalah ni miongoni mwa adabu nzuri. Watunzi wa vitabu wamefahamu kwamba ni miongoni mwa sababu za kutatua haja mbalimbali. Pia imekuja katika Hadiyth iliothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Kila jambo ambalo halianzwi kwa “Alhamduli Allaah” basi halina baraka.”

Bi maana ni lenye baraka kidogo. Kwa hivyo ukisema “Kwa jina la Allaah” au ukasema “Himdi zote njema atashiki Allaah” kisha ndio ukaingia ndani ya maudhui yoyote, basi utakuwa umefuata mwenendo wa wanachuoni katika adabu.

Pindi mtu anapotaka kuandika kitabu, kuandika barua, kutoa Khutbah na mfano wa hayo basi aanze kwa kutaja jina Allaah na kumswalia na kumsalimu Mtume wa Allaah. Baada ya hapo ndio aingie katika makusudio yake. Mwenendo huu ndio uliofuatwa na Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) ambaye ametunga kitabu hiki. Kwa sababu unaposema:

“Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.”

ina maana kwamba umeanza kazi yako hii na uandishi wako kwa kutafuta baraka kwa jina la Muumba ambaye ndiye anastahiki kuabudiwa hali ya kuwa peke yake hana mshirika. Muumba ambaye anasifika kwa sifa kamilifu na tukufu. Miongoni mwa sifa hizo ni sifa ya huruma ilioenea na sifa ya huruma ambayo ni maalum. Sifa ya huruma ilioenea ambayo imefahamishwa na maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنِ

“Mwingi wa rehema.”

Na sifa ya huruma maalum kwa waumini ambayo imefahamishwa na maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحِيمِ

“Mwenye kurehemu.”[1]

[1] 01:03

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 17/11/2021