02. Maana ya msiba na namna ya kukabiliana nao

Allaah (Ta´ala) amesema:

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.” 02:156-157

´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ni neema iliyoje ya mambo mawili yanayochukua nafasi! Ni neema iliyoje ya nyongeza!”

Ameipokea al-Bukhaariy ikiwa na mlolongo wa wapokezi pungufu.

Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ

“Hausibu msiba wowote isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Na yeyote anayemuamini Allaah, Huuongoza moyo wake.” 64:11

´Alqamah na wafasiri wa Qur-aan wengine wamesema:

“Inahusiana na misiba inayompata mtu na akatambua kuwa inatoka kwa Allaah na hivyo akawa ni mwenye kuridhia na kujisalimisha.”

Wasomi wa lugha wanasema kuwa misiba ni kila kile chenye kumuudhi mtu. al-Qurtwubiy amesema:

“Msiba ni kile chenye kumuudhi na kumsibu muumini.”

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote anayepatwa na uchovu, maudhiko, maradhi, huzuni wala hata ile hamu isipokuwa Allaah hufuta madhambi yake kwayo.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna msiba wowote unaompata muislamu hata ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah hufuta madhambi yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 9-11
  • Imechapishwa: 09/10/2016