Hakika Allaah amejaalia mauti kumfika kila mja. Mauti ndio mwisho wa mtu na ndio lengo akiba katika ulimwengu wa maandalizi. Amehukumu na kumfanya aliye na afya njema kuwa mgonjwa na aliye mgonjwa kuwa na afya njema. Amewagawa waja katika mafungu mawili, watiifu na watenda dhambi, na mafikio yao katika nyumba mbili, Peponi na Motoni. Hakuna awezae kuyakimbia mauti. Allaah (Ta´ala) amesema:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ

“Kila aliyekuwa juu yake atatoweka.” 55:26

Hakuna tofauti yoyote kati ya aliye huru na mtumwa, mdogo na mkubwa, tajiri na fakiri. Yote hayo yanatokamana na makadirio ya Aliye mjuzi na mwenye kuyajua mambo yote:

وَمَا يُعَمَّرُ مِن مُّعَمَّرٍ وَلَا يُنقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلَّا فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Na hapewi umri mrefu yeyote mwenye umri mrefu na wala hapunguziwi katika umri wake isipokuwa imo Kitabuni. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” 35:11

Mwerevu ni yule mwenye kujitahidi na akafanyia kazi yaliyo baada ya mauti na yule mwenye maazimio ni yule mwenye kukimbilia kufanya ´amali kabla ya wakati haujaisha. Muislamu ni yule mwenye kujisalimisha na maamuzi makadirio ya Allaah. Muumini ni yule mwenye kuyakinisha kuwa analipwa thawabu kwa subira yake kwa misiba na matatizo.

Ilipokuwa misiba – sawa ya mauti na mingineyo inayopatikana maishani – ni mambo yenye kuumiza na kutia uchungu, nimetaja Hadiyth na mapokezi ambayo yule aliyepatwa na msiba na mwenye subira anayetarajia malipo kutoka kwa Allaah atapata kwavyo fadhila na bishara njema ya Pepo. Baadhi ya Salaf wamesema:

“Lau isingelikuwa ni kwa sababu ya matatizo ya duniani, basi tungelikuwa ni wenye kufilisika siku ya Qiyaamah.”

Hivyo basi, nimependelea kukusanya kitabu ili kuziliwaza nyoyo za wale walio na huzuni na kuwasahilishia wale waliosibiwa. Kitabu nimekipa anwani ya “Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib”, kuwaliwaza wale waliosibiwa na matatizo. Sababu ya kutunga kitabu hichi ni kuwa tauni ilitokea Rajab 775 na ikazidi katika mwisho wa Shawwaal, Dhul-Qa´dah na Dhul-Hijjah. Kikaisha Muharram 776. Maelfu ya watu walifariki na nyumba nyingi zikabaki tupu. Waja wema wengi walifariki kwa tauni hii ikiitwa “tauni bora zaidi” kwa sababu kuna watu wengi wema waliofariki. Lakini hata hivyo wengi iliowasibu ni watoto. Wengi katika marafiki zetu waliokuwa na watoto wengi waliwapoteza watoto wao. Mwaka wa 765 nilitunga kitabu kinachozungumzia tauni na hukumu zake. Ni kitabu kizuri. Hakuna aliyekisoma isipokuwa alikiona kuwa ni kizuri. Ni mara chache kisitaje Hadiyth, mapokezi na historia. Pamoja na hivyo sikutaja kitu katika zile thawabu ambazo Allaah amewaandalia wale wenye kustahamili kwayo. Kwa ajili hiyo ndio maana nimetunga kitabu hichi ili kuwalizawa wale wenye kupatwa na matatizo ya kidunia. Sijapatapo kuwaona wala kusikia kwamba kuna mtu yeyote ambaye hajawahi kupatwa na msiba wowote.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 4-5
  • Imechapishwa: 09/10/2016