Miongoni mwa hukumu zinazoweza kuwa zenye kufichikana kwa baadhi ya watu ni kule kudhania kuwa haifai Tarawiyh kuswaliwa chini ya Rak´ah ishirini na wengine kufikiria kuwa haifai kuswaliwa zaidi ya Rak´ah kumi na moja au kumi na tatu. Dhana zote hizi si za sawa. Bali ni za kimakosa na zinaenda kinyume na dalili. Dalili sahihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinathibitisha kuwa swalah ya usiku inaweza kuswaliwa zaidi ya hivo. Hakuna kiwango maalum ambacho haifai kwenda kinyume nacho. Bali imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anaweza kuswali Rak´ah kumi na moja, Rak´ah kumi na tatu na chini ya hapo katika Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan.

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa juu ya swalah ya usiku alisema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilimbili. Iwapo mmoja wenu atachelea kuingia kwa asubuhi aswali Rak´ah moja ambayo ni Witr kwa yale aliyoswali.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Hakuweka kiwango cha idadi maalum (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Ramadhaan wala isiyokuwa Ramadhaan. Kwa ajili hii ndio maana Maswahabah katika kipindi cha ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) walikuwa wanaweza kuswali Rak´ah ishirini na tatu na wakati mwingine Rak´ah kumi na moja. Yote haya yamethibiti kutoka kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) na kwa Maswahabah katika zama zake.

Baadhi ya Salaf katika Ramadhaan walikuwa wanaswali Rak´ah kumi na tatu na wakimaliza kwa Witr Rak´ah tatu. Wengine walikuwa wakiswali Rak´ah kumi na nne. Haya yametajwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) na wanachuoni wengine. Kadhalika ametaja kwamba suala hili ni pana na kwamba swalah inaweza kuswaliwa kwa njia mbalimbali. Amesema bora kwa ambaye atarefusha kisomo, Rukuu´ na Sujuud apunguze Rak´ah na ambaye atakhafifisha kisomo, Rukuu´ na Sujuud azidishe idadi [ya Rak´ah]. Maneno ya Shaykh-ul-Islaam yana maana kama hii.

Anayetaka kuswali Rak´ah ishirini na amalizie kwa Rak´ah tatu za Witr ni sawa. Anayetaka kuswali Rak´ah kumi na amalizie kwa Rak´ah tatu za Witr ni sawa. Anayetaka kuswali Rak´ah nane na amalizie kwa Rak´ah tatu za Witr ni sawa. Hakuna neno iwapo mtu atapenda kuzidisha au kupunguza kuliko hivo. Hata hivyo lililo bora zaidi ni lile ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya. Alikuwa akiswali R Rak´ah nane na akitoa Tasliym baada ya kila Rak´ah mbili na akimalizia kwa Witr Rak´ah tatu. Alikuwa akisoma kwa unyenyekevu, utulivu na kusoma Qur-aan kwa utungo. Imethibiti katika al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi, si katika Ramadhaan na isiyokuwa hiyo, Rak´ah kumi na moja. Alikuwa akiswali nne [kwanza], usiulize juu ya uzuri na urefu wake. Kisha anaswali nne, usiulize juu ya uzuri na urefu wake. Halafu anaswali tatu.”

Vilevile amepokea al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwake (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku alikuwa akiswali Rak´ah kumi na moja na akitoa Tasliym baada ya kila Rak´ah mbili na akiwitiri kwa Rak´ah moja.

Imethibiti pia kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati mwingine alikuwa akiswali swalah ya usiku Rak´ah idadi ya chini ya hapo. Kadhalika imethibiti ya kwamba wakati mwingine alikuwa anaweza kuswali Rak´ah kumi na tatu na akitoa Tasliym baada ya kila Rak´ah mbili. Hadiyth hizi Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinafahamisha kuwa swalah ya usiku inaweza kuswaliwa kwa njia mbalimbali na himdi zote zinamstahikia Allaah. Hakuna kiwango maalum ambacho hakijuzu isipokuwa hicho tu. Hii ni fadhilah za Allaah, huruma na kuwawepesishia waja Wake na haya yanahusu Ramadhaan na isiyokuwa Ramadhaan.

Bora zaidi kwa ambaye anaswali nyuma ya imamu asitoke isipokuwa baada ya imamu kumaliza swalah yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza ataandikiwa kama ameswali usiku mzima.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min A´maal Ramadhwaan, uk. 04-05
  • Imechapishwa: 30/03/2023