02. Hoja mbalimbali za makinzano kuhusu kupanda kwa imani

Wale wenye kuona kuwa imani ni maneno peke yake pasi na matendo, wamekabiliana na Aayah hizi kwa njia nne:

1 – Msingi wa imani ni kuzitambua zile jumla za faradhi, kama vile swalah na zakaah. Baada ya hapo kuzidi kwake kunahusiana na kuamini kuwa faradhi hizi ni tano, Dhuhr ni Rak´ah nne na Maghrib ni Rak´ah tatu. Vivyo hivyo ndivo wanavyoyaona mambo mengine yaliyo faradhi.

2 – Msingi wa imani ni kutambua yale yaliyokuja kutoka kwa Allaah na kuzidi kwake ni kutendea kazi kutambua huko.

3 – Kuzidi kwa imani inahusiana na kuzidi kwa yakini.

4 – Imani haizidi hata siku moja lakini watu wanazidi kutokana nayo.

Sijamuona mwanachuoni yeyote akithibitisha tafsiri yoyote katika hizi wala hayana msingi wowote katika lugha ya kiarabu. Kufasiri maneno yake Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) “Keti nasi tuumini kitambo kidogo” kwa njia zilizotajwa hapo juu kunaweza kumfanya mtu kufikiria kuwa mtu kama yeye hakuwa anajua idadi ya zile swalah tano na Rukuu´ zake na Sujuud zake isipokuwa baada ya kufari kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimfadhilisha mbele ya Maswahabah zake wengi inapokuja katika kuyatambua yaliyo halali na yaliyo haramu kisha akasema:

“Pindi wanazuoni watapohudhuria mbele ya Mola Wao (´Azza wa Jall), Mu´aadh bin Jabal atakuwa amewatangulia kwa kiasi cha kurusha mshale.”[1]

Hakuna yeyote anayemjua Mu´aadh ataweza kufasiri namna hiyo.

Hata katika lugha ya kiarabu sijapata chochote kinachosapoti tafsiri zao. Hilo ni mfano wa mtu ambaye amekubali kuwa amemkopesha dirhamu 1 000 mtu mwingine, baada ya hapo akabainisha kuwa amegawa 100 upande fulani, 200 upande fulani mpaka zikakamilika 1 000. Hilo haliitwi kuzidi; hilo huitwa kumjulisha na kupambanua. Hata kama asingejumlisha pesa hizo lakini akakariri kutambua huko mara nyingi, bado lisingezingatiwa kuwa ni kuzidi – lingezingatiwa ni kukariri na kurudiarudia. Kwa sababu maana inabaki ni ileile na hakuzidisha kitu.

Kuhusu wale waliosema kuwa imani hata siku moja haizidi lakini watu wanazidi kutokana nayo, ´Aqiydah hiyo haipo. Kwa sababu mtu akisema kuwa yuko na pesa 1 000 na baadaye kumezidi pesa 100, hakuna wanachofahamu watu isipokuwa ni kwamba hivi sasa ana pesa 1 100. Vivyo hivyo ndivo yalivyo mambo mengine yote, kukiwemo imani. Hakuna chochote kinachozidi kwa watu isipokuwa kitu hichohicho ndio kimezidi katika imani.

Nadharia inayosema kuwa kuzidi kunakuwa katika yakini haina maana yoyote. Kwani yakini ni katika imani. Ikiwa wanaona kuwa imani yote ni kule kutambua peke yake kisha watu hawa wanaokiri wakaikamilisha kwa kule kukiri kwao, basi ni lazima wawe wameizunguka kwa yakini. Kitu ambacho kimeshachimbwa na kuzungukwa kinawezaje kupanda zaidi? Mnasemaje mtu ambaye anawatazama watu wakati wa asubuhi wakati kuna mwanga mkubwa; je, yakini yake inaweza kuzidi ya kwamba ni mchana hata kama atakusanyikiwa na watu na majini? Hili ni jambo lisilowezekana kabisa na linatoka nje ya yale wanayoyatambua watu.

[1] Ameipokea Ibn Sa´d kupitia kwa Muhammad bin Ka´b na al-Hasan al-Baswriy pasi na Swahabah katika cheni ya wapokezi wake. Yeye na na Ibn ´Asaakir wameipokea kutoka kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh). al-Haakim ameipokea kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh). at-Twabaraaniy ameipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hadiyth ni Swahiyh kutokana na mkusanyiko wa njia zake.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 45-49
  • Imechapishwa: 25/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy