Imaam ´Abdul-Ghaniy bin ´Abdil-Waahid al-Maqdisiy (Rahimahu Allaah) amesema:

195 – Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

”Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) katika safari moja. Miongoni mwetu wako waliofunga na miongoni mwetu wengine hawakufunga. Tukatua mahali katika siku yenye joto na wengi wetu tulikuwa tunaegama kivuli kwa ambaye alikuwa na kitambaa. Miongoni mwetu wako wanaozuia jua kwa mikono yao. Wafungaji wakadondoka na wasiofunga wakainuka na kujenga majengo na wakawanywesha maji wanyama. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) akasema:

”Wasiofunga leo wameondoka na thawabu.”[1]

196 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Nilikuwa na deni la swawm ya Ramadhaan na siwezi kuilipa isipokuwa katika Sha´baan.”[2]

197 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) amesema:

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”[3]

Ameipokea Abu Daawuud na akasema:

“Hili linahusu katika nadhiri tu. Vilevile ndio maoni ya Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah).”

MAELEZO

Hadiyth hizi tatu moja wapo inahusiana na kufunga safarini. Nayo ni ile Hadiyth ya Anas (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

”Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) katika safari moja. Miongoni mwetu wako waliofunga na miongoni mwetu wengine hawakufunga. Tukatua mahali katika siku yenye joto na wengi wetu tulikuwa tunaegama kivuli kwa ambaye alikuwa na kitambaa. Miongoni mwetu wako wanaozuia jua kwa mikono yao. Wafungaji wakadondoka na wasiofunga wakainuka na kujenga majengo na wakawanywesha maji wanyama. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) akasema:

”Wasiofunga leo wameondoka na thawabu.”

Hii inajulisha juu ya ubora wa kula safarini na khaswa kipindi cha joto kali. Katika hali hiyo ni bora zaidi kuliko kufunga. Jengine mtu anapaswa kukubali ruhusa ya Allaah. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi atimize idadi katika masiku mengine..”[4]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam):

“Sio katika wema kufunga safarini.”

Bi maana sio katika wema timilifu kufunga safarini. Bali bora ni kula.

”Allaah anapenda itendewe kazi ruhusa Yake kama anavochukia kuendewa maasi Yake.”[5]

Joto likiwa kali basi kunasisitizwa kuacha kufunga ili kila mmoja aweze kusimamia mahitaji na kazi yake na pia apate uchangamfu wa kuwahudumia ndugu zake. Lakini akifunga na wengine wakala basi anakuwa mzigo kwa ndugu zake na anakuwa ni taabu kwao kutokana na kule kushindwa kwake na nyonge wake. Isitoshe ukweli wa mambo ni kwamba hakukubali ruhusa hii ambayo ndani yake Allaah amemneemesha, kumtendea wema na kumfanyia upole. Kwa hiyo anatakiwa kuikubali.

[1] al-Bukhaariy (2890) na Muslim (1119).

[2] al-Bukhaariy (1950) na Muslim (1146).

[3] al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147).

[4] 02:185

[5] Ahmad (5866), at-Twabaraaniy (8032),  Ibn Hibbaan (354) na Ibn Khuzaymah (03/259) na Abu Nu´aym (06/276). Shaykh al-Albaaniy amesema:

”Nzuri na Swahiyh.” (Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (01/256)).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ifhaam fiy Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/403-404)
  • Imechapishwa: 17/03/2022