Imaam ´Abdul-Ghaniy bin ´Abdil-Waahid al-Maqdisiy (Rahimahu Allaah) amesema:

191 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kwamba Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy alisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Nifunge safarini?” Akamjibu: ”Ukitaka funga na ukitaka acha kufunga.”[1]

192 – Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Tulikuwa tukisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yule mwenye kufunga hakumkosoa yule ambaye hakufunga na yule ambaye hakufunga hakumkosoa yule ambaye amefunga.” [2]

193 – Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Tulisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mwezi wa Ramadhaan wakati ambapo kulikuwa na joto kali kiasi cha kwamba kuna ambao walikuwa wakiweka mkono kichwani kutokana na ukali wa joto. Hakuna kati yetu ambaye alikuwa amefunga isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaahah.”[3]

194 – Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa safarini ambapo akaona msongamano na mtu ambaye amefanyiwa kivuli. Akasema: “Mambo gani haya?” Wakasema: “Amefunga.” Akasema: “Sio katika wema kufunga safarini.”[4]

Tamko la Muslim limekuja likisema:

“Jilazimieni na ruhusa ya Allaah ambayo amekuruhusini.”[5]

MAELEZO

Hadiyth hizi nne zinahusiana na kufunga safarini. Hadiyth Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) zimejulisha – kama ilivyofahamisha Qur-aan pia – ya kwamba hapana neno kufunga safarini kama ambavo hapana neno pia kuacha kufunga na kwamba ni ruhusa ya Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (´Azza wa Jall):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi atimize idadi katika masiku mengine.”[6]

Bi maana akala basi analazimika kutimiza idadi katika masiku mengine. Kwa hiyo msafiri ana khiyari; akitaka kufunga atafunga, na akitaka kuacha kufunga atakula. Isipokuwa ikiwa safari iko na ugumu na uzito. Katika hali hiyo inapendeza kwake kula na imechukizwa kwake kufunga kutokana na ule ugumu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam):

“Sio katika wema kufunga safarini.”

Sio katika wema timilifu kufunga safarini. Hapo ilikuwa wakati alipomuona bwana mmoja ametengenezewa kivuli na watu wamesongamana kwake kutokana na ile tabu anayopata. Akachukizwa (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) na kufunga na ndipo akasema:

”Sio katika wema… ”

Wema timilifu.

”… kufunga safarini.”

Sio katika wema mtu kufunga safarini ikiwa kuna uzito na ugumu. Hivi ndivo zinaoanishwa Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam). Kwa ajili hiyo Hadiyth ya kwanza ya Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy alimwambia:

”Ukitaka funga na ukitaka acha kufunga.”

Imekuja katika tamko jengine:

”Ni ruhusa ya Allaah. Yule anayetaka kuitendea kazi ni vizuri na anayependa kufunga basi hakuna dhambi kwake.”

Katika Hadiyth ya Anas ameeleza kwamba walikuwa wakisafiri pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) na aliyefunga hamsemi vibaya ambaye hakufunga na kinyume chake. Walikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam). Mara (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) alikuwa akila na mara akifunga[7].

Katika Hadiyth ya Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba walisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika kipindi cha joto kali na walikuwa wenye kula na hakuna aliyefunga isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaahah. Safari ilikuwa ngumu. Haya pengine yalitokea pale mwanzoni kabla ya kuteremka Wahy katika hali ya kuhisi ugumu. Kwa hiyo Hadiyth ya Abud-Dardaa´ itafasiriwa kwamba ilikuwa pale mwanzoni. Baadaye Allaah akateremsha wepesi, usahilishaji na mahimizo ya kula safarini ikiwa kuna uzito kutokana na Hadiyth ya Jaabir. Namna hii ndio yanaoanishwa maelezo. Ikiwa kuna uzito basi imechukizwa kwao kufunga na imesuniwa kwao kula kwa masisitizo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) amesema:

“Sio katika wema kufunga safarini.”

Bi maana sio katika wema timilifu kufunga safarini au sio katika wema kufunga safarini ikiwa kipindi ni cha joto kali kinachomtaabisha muumini. Lakini ikiwa kipindi sio kigumu basi mtu yuko na khiyari; akitaka kufunga basi atafunga, na akitaka kuacha kufunga basi atakula ingawa katika hali zote kula ndio bora zaidi kutokana na ueneaji wa:

“Sio katika wema kufunga safarini.”

Kwa hivyo kula ndio bora zaidi kwa sababu mtu anakubali ruhusa ya Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam):

”Allaah anapenda itendewe kazi ruhusa Yake.”[8]

Amesema katika Hadiyth ya Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy iliopokelewa na Muslim:

”Ni ruhusa ya Allaah. Yule anayetaka kuitendea kazi ni vizuri na anayependa kufunga basi hakuna dhambi kwake.”[9]

Ikafahamisha kwamba hapana dhambi kufunga ingawa kula ndio bora zaidi.

Isitoshe mara nyingi msafiri huathirika kwa kule kufunga na inamtaabisha. Hata kama sio katika kipindi cha joto kali akiacha kufunga ndio bora zaidi na akifunga hapana neno kwake. Katika kipindi cha joto kali na kujikakama itasuniwa kwake kula na itasisitizwa kwake kula.

[1] al-Bukhaariy (1943) na Muslim (1121).

[2] al-Bukhaariy (1947) na Muslim (1118).

[3] al-Bukhaariy (1945) na Muslim (1122).

[4] al-Bukhaariy (1946) na Muslim (1115).

[5] Muslim (1115).

[6] 02:185

[7] al-Bukhaariy (1947) na Muslim (1118).

[8] Ahmad (5866), at-Twabaraaniy (10030),  Abu Nu´aym (02/101). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa´-ul-Ghaliyl” (03/09).

[9] Muslim (1121).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ifhaam fiy Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/398-401)
  • Imechapishwa: 17/03/2022