02. Hadiyth kuhusu Yaa Siyn kwa anayekata roho ni dhaifu

Swali 02: Je, inafaa kusoma ”Yaa Siyn” kwa anayetaka kukata roho[1]?

Jibu: Kusoma Suurah ”Yaa Siyn” mbele ya anayetaka kukata roho ni jambo limetajwa katika Hadiyth ya Ma´qil bin Yasaar ambaye amesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Wasomeeni maiti wenu Yaa Siyn.”[2]

Wameisahihisha kikosi cha wanazuoni na wakafikiri kuwa cheni ya wapokezi wake ni nzuri na kwamba ni katika upokezi wa Abu ´Uthmaan an-Nahdiy kutoka kwa Ma´qil bin Yasaar. Wapo wanazuoni wengine walioidhoofisha na wakasema kuwa mpokezi wake sio Abu ´Uthmaan an-Nahdiy na kwamba ni mtu mwengine asiyejulikana. Hadiyth ni dhaifu kutokana na kutotambulika Abu ´Uthmaan. Kwa hivyo haikupendekezwa kumsomea nayo maiti. Waliopendekeza jambo hilo walifikiri kuwa Hadiyth ni Swahiyh na hapo ndipo wakapendekeza jambo hilo. Lakini kusoma Qur-aan mbele ya maiti ni jambo zuri na pengine Allaah akamnufaisha kwayo. Kuhusu kufanya maalum Suurah “Yaa Siyn” msingi ni kwamba Hadiyth ni dhaifu na hivyo kufanya maalum hakuna mashika yoyote.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/93).

[2] Ahmad (19790) na Abu Daawuud (3121).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 10/12/2021