02. ´Aqiydah sahihi juu ya Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat

Miongoni mwa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni pamoja na kwamba wanathibitisha majina mazuri mno na sifa kuu ambazo Allaah (Ta´ala) amejithibitishia Mwenyewe na ambazo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemthibitishia. Hawavuki Qur-aan na zile Hadiyth zilizothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Wanathibitisha hayo kimatamshi na wanatambua maana yake katika lugha ya kiarabu ambayo Qur-aan imeteremshwa kwayo. Hata hivyo namna yake wanamwachia Allaah (Ta´ala), kwa kuwa ni maalum kwa Allaah (Ta´ala) na hakuna mwengine yeyote mwenye ujuzi kwayo.

Katika mlango huu wa khatari wanatokea kwenye misingi ya Kishari´ah iliyothibiti; yule mwenye kushikamana nayo basi anasalimika na upindaji.

Wa kwanza: Kuthibitisha yale ambayo Allaah (Ta´ala) amejithibitishia nayo katika nafsi yake na yale ambayo Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemthibitishia. Haya yanatakiwa kufanyika pasi na kuongeza wala kupunguza, kwa kuwa hakuna yeyote ambaye ni mjuzi wa kumtambua Allaah (Ta´ala) kuliko anavojijua Mwenyewe:

قُلْ أَأَنتُمْ أَعْلَمُ أَمِ اللَّـهُ

“Je nyinyi mnajua zaidi au Allaah?” (02:140)

Hakuna mwanadamu yeyote ambaye ni mjuzi wa kumtambua Allaah kuliko Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

“Na wala hatamki kwa matamanio yako – hayo ayasemayo si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa kwake.” (53:03-04)

Wa pili: Kumtakasa Allaah (Ta´ala) kutokamana na kushabihiana na sifa za viumbe. Allaah (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala haiwi awe na yeyote anayefanana na kulingana Naye.” (112:04)

Wa tatu: Mtu asijaribu kufikiria sifa Zake. Allaah (Ta´ala):

وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Na wala wao hawawezi kuzunguka elimu Yake.” (20:110)

هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا

“Je, unamjua mwengine mwenye jina kama Lake?” (19:65)

Miongoni mwa sifa hizi ni pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Haya yametajwa sehemu nyingi katika Qur-aan. Hapa mtu anatakiwa kuelewa ya kwamba kulingana kwa Allaah juu ya ´Arshi ni kulingana kikweli. Tunaelewa maana yake na hatujui namna yake. Maana yake ni kuwa juu na kungatika. Haya ndio yenye kufahamishwa na lugha ya kiarabu. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wamekubaliana juu ya maana hii. Kuhusiana na namna ya kulingana huku, hakuna yeyote anayeijua isipokuwa Allaah peke yake, hali ya kuwa hana mshirika.

Hali kadhalika Allaah (Ta´ala) anasema:

إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا

“Hakika Allaah daima ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (04:58)

Hapa kunathibitishwa usikivu wa Allaah. Kwa mujibu wa lugha ya kiarabu usikivu maana yake ni “kuifikia sauti”.

Tunamthibitishia Allaah (Ta´ala) usikizi ambao anazifikia kwao sauti. Usikivu huu haufanani na usikivu wa viumbe vya Allaah. Kuhusu namna yake, tunamwachia Allaah (Ta´ala). Hivyo hatusemi: “Anasikia vipi?” Hatujiingizi katika hilo, kwa kuwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hakutufanya tujue hilo. Bali ni katika mambo ambayo Allaah (Jalla wa ´Alaa) peke yake ndiye mwenye ujuzi kwayo.

Vivyo hivyo inahusu uoni; kufikia vyenye kuonwa. Imethibiti katika “as-Swahiyh” ya Muslim kutoka kwa Abu Muusa al-Ash´ariy ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah halali na wala haimstahikii Yeye kulala. Anainyanyua mizani kuishusha. Kwake hupanda matendo ya usiku kabla ya matendo ya mchana na matendo ya mchana kabla ya matendo ya usiku. Pazia Yake ni Nuru; lau ataifunua, basi mwanga wa uso Wake ungeliunguza kila akionacho katika viumbe Wake.”

Tunamthibitishia Allaah uoni wa kihakika ambao kwao anafikia vyenye kuonwa. Pamoja na kwamba hatuna ujuzi wowote kuhusu namna ya uoni huu. Sisi tunajua yale ambayo Allaah ametujuza kwa kusema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”

Hii ni baadhi ya mifano ya namna ambavyo Ahl-us-Sunnah wanaamini majina na sifa za Allaah.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 17-20
  • Imechapishwa: 20/06/2020