02. Anayepuuza swalah ataandamana na hawa siku ya Qiyaamah

Ni jambo linalojulikana kwamba swalah ndio nguzo ya Uislamu na nguzo ya pili miongoni mwa nguzo zake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kichwa cha mambo ni Uislamu, nguzo yake ni swalah na jihaad katika njia ya Allaah ndio nundu yake ya juu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema tena katika Hadiyth Swahiyh:

“Uislamu umejengwa juu ya matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji nyumba ya Allaah.”[2]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatajia fadhilah za swalah ambapo akasema:

“Yeyote atakayeichunga basi atakuwa na nuru, hoja na uokozi siku ya Qiyaamah. Na yeyote ambaye hatoichunga basi hatakuwa na nuru, hoja na uokozi. Aidha siku ya Qiyaamah atakuwa na Qaaruun, Fir´awn, Haamaan na Ubay bin Khalf.”[3]

Hadiyth hii Swahiyh inahusu swalah ya ijumaa na nyenginezo katika zile swalah tano. Ndani yake mna ahadi kubwa kwa ambaye ataihifadhi na akanyooka juu yake ya kwamba atakuwa na nuru duniani na Aakhirah, hoja na uokozi siku ya Qiyaamah. Sambamba na hayo kuna matishio makali kwa ambaye hatoichunga ya kwamba hatokuwa na nuru, hoja na uokozi. Aidha siku ya Qiyaamah atafufuliwa na Fir´awn, Haamaan, Fir´awn na Ubay bin Khalf. Haya yanahusu zile swalah tano kwa sura ilioenea na swalah ya ijumaa kwa sura maalum. Aidha yanakusanya kuitekeleza ndani ya wakati wake kama Allaah alivoweka katika Shari´ah na katika mkusanyiko pamoja na waislamu.

Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametaja kwamba mpoteza swalah atafufuliwa pamoja na makafiri hawa ambao ndio walinganizi wa ukafiri na upotofu na ambao ndio viongozi wa ukafiri kwa ajili ya kutahadharisha jambo hili na kufanya watu walikimbie ili muislamu asijifananishe na makafiri hawa. Kwa sababu akiipoteza kwa sababu ya uongozi na ufalme, basi amefanana na Fir´awn ambaye aliponzwa na ufalme na uongozi wake mpaka akachupa mpaka na kupindukia na kufikia kusema:

أنا ربكم الأعلى

“Mimi ndiye Mola wenu mkuu.”[4]

Matokeo yake akaingia Motoni. Kwa hiyo haitakikani kwa muumini kujifananisha na kiongozi huyu mpotofu na kafiri. Akijifananisha naye na uongozi wake ukamshughulisha na yale ambayo Allaah amemuwajibishia, basi atafufuliwa pamoja naye kuelekea Motoni.

Akipoteza swalah kwa sababu ya mambo ya wizara na kazi, basi amefanana na Haamaan ambaye alikuwa waziri wa Fir´awn. Matokeo yake siku ya Qiyaamah atafufuliwa pamoja naye kuelekea Motoni.

Akipoteza swalah kwa sababu ya mali, mambo ya matamanio na kuiridhisha nafsi, basi amefanana na Qaaruun ambaye alikuwa mfanyabiashara wa wana wa israaiyl na ambaye alikuwa dhalimu wao aliyechupa mpaka, akapindukia na akamuasi Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kufanya kiburi. Allaah akamdidimiza yeye na nyumba yake ardhini. Yeyote atakayejifananisha naye, basi atafufuliwa naye siku ya Qiyaamah.

Akijishughulisha na biashara basi amefanana na Ubay  bin Khalaf ambaye alikuwa mfanyabiashara wa watu wa Makkah. Matokeo yake atafufuliwa naye kuelekea Motoni. Tunamwomba Allaah ulinzi kutokamana na hayo.

[1] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[2] Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim, ambaye pia kaipokea.

[3] Ahmad (6288) na ad-Daarimiy (2605).

[4] 79:24

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 29/11/2021