01. Mambo ya kidunia yasimghulishe mtu na yale Allaah aliyowajibishiwa

Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee mtukfuu wa Mitume.

Wa ba´d:

Hakika ijumaa kunatafutwa unyenyekevu na utulivu ili kuhudhuria kheri hii na kushiriki ndani yake katika kuswali na kumtaja Allaah na kusikiliza yale yanayokunufaisha katika jambo la dini na dunia yako. Allaah (Subhaanah) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya swalah siku ya ijumaa, basi kimbilieni kumtaja Allaah na acheni biashara. Hivyo ni kheri kwenu mkiwa mnajua.”[1]

Baada ya hapo akaamrisha (Subhaanah) yale yanayomnufaisha mtu katika dunia na Aakhirah. Akasema:

فَإِذَا قُضِيَتِ الصَّلَاةُ فَانتَشِرُوا فِي الْأَرْضِ وَابْتَغُوا مِن فَضْلِ اللَّـهِ وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“Inapomalizika swalah, basi tawanyikeni katika ardhi na tafuteni katika fadhilah za Allaah na mtajeni Allaah sana ili mpate kufaulu.”[2]

Bi maana tafuta riziki na kheri:

وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

“… na mtajeni Allaah sana ili mpate kufaulu.”[3]

ili msishughulishwe na aina mbalimbali za biashara, ladha na mahitaji ya kidunia kutokamana na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na sababu za kufaulu. Kufaulu kuko ndani ya kumtaja Allaah na kutekeleza maamrisho ya Allaah. Kwa hiyo mahitaji ya mwili hayatakiwi kutawala mahitaji ya moyo na ya roho. Kama ambavo mahitaji ya moyo na roho hayatakiwi kutawala mahitaji ya mwili na ya dunia. Kila kimoja kinatakiwa kuchungwa vyema. Waislamu wanatakiwa kutekeleza yote mawili. Wakati fulani inakuwa katika mambo ya dunia na mahitaji yao; huyu anafanya kazi ya kilimo katika shamba lake, mwingine katika duka lake, mwingine katika mahitaji na kazi nyingine miongoni mwa zile kazi alizohalalisha Allaah (´Azza wa Jall). Lengo ni ili watu wote washiriki katika miradi ya hisani na kazi zilizohalalishwa na zenye kuleta manufaa. Lengo jengine ni masikini wafarijiwe na watu wengine wafanyiwe wema.

Zinapofika nyakati ambazo Allaah amemuwajibisha mtu jambo, basi anakimbilia kumtii Allaah na kutekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia. Kwa msemo mwingine mahitaji yasimshughulishe na mahitaji mengine. Badala yake aipe kila nafasi kile kinachostahiki na aipe kila haja kile kinachonasibiana nayo. Anakuwa ni mwenye kuchunga wakati wake na anatekeleza yale ambayo Allaah amemuwajibishia hali ya kuwa ni mwenye kutafuta riziki na akihangaika juu ya ardhi ya Allaah akiitafuta halali.

[1] 62:09

[2] 62:10

[3] 62:10

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 29/11/2021