01. Utangulizi wa mtunzi wa “Sharh Usuwl-ith-Thalaathah”

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah, amani na baraka zimwendee mja na Mtume Wake Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote na wale watakaomfuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

Ama baada ya hayo;

Miongoni mwa vitabu vya Imaam na Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) ambavyo vimekubaliwa na wanazuoni wa ummah na wanafunzi kwa hali ya kushangaza ni kitabu hiki kilichoko mbele yetu. Nacho ni ”Usuwl-uth-Thalaathah”. Misingi hiyo mitatu aliyoitaja (RahimahuAllaah) ni kama ifuatavyo:

1 –Mja kumtambua Mola Wake.

2 – Mja kutambua Uislamu kwa dalili.

3 – Kumtambua Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Misingi hii mitatu ndio ambayo mtu ataulizwa nayo pale atapolazwa ndani ya kaburi lake. Nayo ndio ambayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameitaja pale aliposema:

”Husikia nyayo za viatu vya watu wake wanapogeuka kuondoka zao. Humjilia mwenye kumjilia na kumuuliza: ”Ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako?” Husema: ”Mola wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Mtume wangu ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Humkemea na kumuuliza tena: ”Ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako?” Hii ndio fitina ya mwisho atayoonyeshwa muumini.

Kuhusu kafiri au mnafiki ataulizwa ni kipi alichokuwa anasema kuhusu bwana huyu? Atajibu: ”Sijui. Nilikuwa nasema yale wasemayo watu.” Ataambiwa: ”Hukujua na wala hukusoma.” Kisha atapigwa nyundo ya chuma kati ya masikio yake ambapo akapiga kelelezitazosikiwa na viumbe wote isipokuwa watu na majini.” Imepokelewa katika upokezi mwingine: ”Kaburi lake litambana mpaka zikutane mbavu zake.”[1] Hayo yamethibiti katika Hadiyth Swahiyh.

Misingi hii mitatu aliyoandika imaam ni kitabu kitukufu. Ndio maana kitabu hiki kikawa kinahifadhiwa. Anakihifadhi mwanafunzi mdogo na mkubwa. Hakuna mwenye kujitosheleza nacho. Kinasomeshwa katika mashule na misikiti. Ni miongoni mwa vitabu vya mwanzo kabisa ambavyo mwanafunzi anatakiwa kuanza navyo katika somo linalohusu ´Aqiydah. Anatakiwa kuanza kusoma ”al-Usuwl ath-Thalaathah”, ”al-Qawaa´id al-Arba´ah”, ”Nawaaqidh-ul-Islaam”, ”Kashf-ush-Shubuhaat”, kisha apande daraja kwenda ”Kitaab-ut-Tawhiyd”, ”al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah” vya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, kisha ”al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah”, ”al-´Aqiydah al-Hamawiyyah”, ”at-Tadmuriyyah”, kisha vitabu vya Sunnah kama vile ”Usuwl-us-Sunnah” cha Imaam Ahmad, ”as-Sunnah” cha mwanawe ´Abdullaah, ”as-Sunnah” cha al-Khallaal, ”Sharh-us-Sunnah” cha al-Barbahaariy na venginevyo.

Mtunzi ambaye ni Imaam na Mujaddid (Rahimahu Allaah) ameleta mtindo wa kielimu na wa kimsingi ambao anaufahamu kila mtu. Sio mtindo wa kutaka kujaza, mgumu, kukariri wala kuzidisha. Kila neno analozungumza basi analiandamishia dalili. Kwa sababu maneno hayasihi isipokuwa kwa dalili. Aidha kufanya hivo kunathibitisha elimu zaidi na kusimamisha zaidi hoja.

Mimi nawashauri wanangu na ndugu zangu watilie umuhimu kitabu hiki hali ya kukifunza wadogo na wakubwa na pia wafahamu maana yake. Uzuri uliyoje iwapo watafanyiwa maelezo mafupi au wa kati na kati kwa kutegemea viwango vya wale wanafunzi. Lakini mtu akitaka kuzama zaidi kukipambanua basi yatakuja maelezo yake katika juzu kadhaa kutokana na ile elimu na dalili zilizomo ndani yake. Maelezo hayo yatakuwa na matamshi mafupi na yenye maana yenye kutosheleza.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Imeandikwa na;

´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy

[1] Abu Daawuud (4753), Ahmad (12271) na al-Haakim (107). al-Haakim amesema:

“Ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye. Ameisahihisha pia Ibn-ul-Qayyim katika “I´laam-ul-Mu´aqqi´iyn” (01/137).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 09-11
  • Imechapishwa: 30/01/2023