01. Ulazima wa baba na mama kusaidiana katika wema na kumcha Allaah

Swali 01: Nina watoto kuanzia miaka tisa mpaka ishirini na tano ambao hawaswali pamoja na mkusanyiko siku zote. Mimi nawaamrisha, nawagombeza na nawaamsha kutoka usingizini wakiwa wamelala na baada ya hapo wanaingia bafuni kutawadha. Kisha humwomba mama yao kukamilisha kazi hiyo na awahimize kutoka haraka kwa ajili ya kwenda kuswali msikitini. Lakini hawahudhurii msikitini siku zote na khaswa katika swalah ya Fajr. Hali hii ni pale ninapokuwa kwao. Lakini ninapokuwa katika nyumba nyingine – kwa sababu mimi nimeoa mwanamke mwingine – basi hawahudhurii msikitini isipokuwa mara chache. Nimemwomba mama yao kuwaamrisha kuswali pamoja na mkusanyiko na akamilishe yale niliyoyaanza kwa sababu mimi huwaamsha na hutoka ilihali wao wako bafuni. Aidha nimemwomba awasimamie ninapokuwa sipo na atumie vitisho na pengine wakati mwingine kipigo hali ikipelekea kufanya hivo. Lakini hata hivyo hafanyi hivo. Je, una nasaha zozote za kuwapa wao na yeye mama khaswa kwa kuzingatia kwamba anasema kuwa ni jukumu langu mimi na sio jukumu lake yeye. Je, maneno haya ni sahihi[1]?

Jibu: Ni wajibu kwako, kwao na juu ya mama yao kusaidiana katika wema na kumcha Allaah na kutumia sababu zinazowezekana kuswali katika mkusanyiko japo ni kwa wewe au mama yao kuwapiga kwa yule ambaye amefikisha miaka isiyopungua kumi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapokuwa na miaka saba  na wapigeni kwayo wanapofikisha miaka kumi na pia watenganisheni katika malazi.”[2]

Allaah (Subhaanah) amesema:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ

“Waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao; wanaamrisha mema na wanakataza maovu.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote katika nyinyi mwenye kuona maovu, basi ayazuie kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa kuzungumza. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake.”[4]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayesikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”[5]

Akaulizwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa): “Ni udhuru upi?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Zipo Aayah na Hadiyth nyingi juu ya maudhui haya. Namwomba Allaah atengeneze dhuriya yetu na dhuriya yenu na dhuriya ya waislamu wote, akusaidie wewe na mama yako kwa kila kilicho na matengenezo kwa wote na kutakasika kwa dhimma. Kwani hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa, Mkarimu.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/22-23)

[2] Ahmad (6716) na Abu Daawuud (495).

[3] 09:71

[4] Muslim (70) na an-Nasaa´iy (4922).

[5] Ibn Maajah (785).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 19-21
  • Imechapishwa: 22/11/2021