Haya ni miongoni mwa matatizo ya kifamilia yanayogubika jamii ya kiislamu na jambo hili huzidi kutegemea wakati na watu kwa kiasi cha miji na hali za watu. Kabla ya kuanza kuzungumzia sababu za talaka nataka kuanza na utangulizi. Nasema:

Namzungumzisha muislamu wa kiume na muislamu wa kike nikiwa ni mwenye kuwaandikia kijitabu hiki pengine Allaah akatunufaisha sote. Talaka ni tatizo la kijamii na leo imekuwa katika baadhi ya miji ni sura ya kifamilia ambayo inasumbua familia za watu. Talaka ni kitu gani? Ni zipi sababu zake? Je, talaka ni shari tupu? Ni ipi tiba ya talaka? Haya ni mambo mengi ambayo nimeandika juu yake yale ambayo Allaah amenifungulia. Allaah ndiye mwenye kuwafikisha na mwenye kuongoza katika njia ilionyooka. Mambo hayo nitayagawanya sehemu mbalimbali ili nisimfanye msomaji ni mwenye kuchoka.

Sababu za talaka na tiba yake:

Maana ya talaka kwa mujibu wa lugha ni kuondosha kile kifungu kwa hali yoyote. Ni jambo limechukuliwa kutoka katika kumwachilia ngamia (إطلاق البعير) ambapo ni kule kumfungua na ile kamba yake. Akiachwa na kufunguliwa kutoka katika ile kamba yake, basi huachika. Hii ndio maana ya kuondosha kile kifungu kwa hali yoyote. Kwa mujibu wa Shari´ah zote zina maana moja. Ni kule kuondosha kile kufungu cha ndoa na kumaliza yale mahusiano ya ndoa ima kabisa au kwa njia ya kurejea bila badali yoyote kwa tamko maalum na la wazi. Kwa mfano mwanamme kusema ´wewe umeachika`. Inaweza vilevile ikawa kwa fumbo. Kwa mfano mwanamme kusema ´wewe ni mwenye kuachika` au ´nenda kwa familia yako`. Yote haya ni mafumbo. Talaka inaweza vilevile ikawa kwa njia ya kuashiria. Hili linaweza kufanywa na yule mwanamme asiyeweza kuzungumza au kuandika. Katika kikao hichi hatutozungumzia hukumu za talaka kama vile ni wakati gani inapita, wakati gani haipiti, matamshi yake yanayopendeza, matamshi yake yasiyopendeza, talaka rejea, talaka isiyokuwa rejea, talaka inayoafikiana na Sunnah na talaka isiyoafikiana na Sunnah. Mada yetu tutazungumzia sababu za talaka. Huu ni utangulizi tu nimependa uanze kabla ya maudhui yetu usiku huu.

ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Talaka ndani ya Qur-aan imekuja kwa majina matatu:

1 – Talaka.

2 – Kufarikiana.

3 – Kuachana.

Allaah (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ

“Ee Nabii!  Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa twahara zao.”[1]

Hii ni talaka.

Amesema (´Azza wa Jall):

فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ فَارِقُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ

“Atakapokaribia kufikia muda wao, basi wazuieni kwa wema au farikianeni nao kwa wema.”[2]

Huku ni kufarikiana.

Amesema kumwambia Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya wakeze:

إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا

”Ikiwa mnataka maisha ya dunia na mapambo yake, basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru kuachana kuzuri.”[3]

Huku ni kuachana.

Je, talaka ni jambo limewekwa katika Shari´ah? Hapana shaka kuwa talaka ni jambo linakubalika kwa mujibu wa Shari´ah kwa dalili ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Allaah (Ta´ala) amesema.

وَإِنْ عَزَمُوا الطَّلَاقَ فَإِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Wakiazimia talaka, basi hakika Allaah ni Msikivu wa kila kitu, Mjuzi wa yote.”[4]

الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ ۖ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ

”Talaka ni mara mbili. Hivyo kuzuia kwa mujibu wa Shari´ah au kuachia kwa wema.”[5]

وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللَّـهُ كُلًّا مِّن سَعَتِهِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ وَاسِعًا حَكِيمًا

“Wakifarikiana basi Allaah atampa utajiri kila mmoja katika wasaa Wake; na Allaah ni Mwenye wasaa, Mwenye hekima.”[6]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ

“Enyi walioamini! Mnapofunga ndoa na waumini wa kike kisha mkawataliki… ”[7]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwataliki baadhi ya wakeze pasi na kuwarejea na wengine akawarejea. Miongoni mwao ni Hafswah bint ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu  ´anhumaa)[8].

[1] 65:01

[2] 65:02

[3] 33:28

[4] 02:227

[5] 02:229

[6] 04:130

[7] 33:49

[8] al-Haakim (04/16) (6753) ambaye amepokea kupitia kwa Qays bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtaliki Hafswah bint ´Umar. Baadaye wakaja wajomba zake (Qudaamah na ´Uthmaan – watoto wa Madh´uun) ambapo Hafswah akaanza kulia. Hajanitaliki kwa sababu ya kunichukia. Akaja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: ”Mrejee Hafswah, kwani hakika ni mwanamke mwenye kufunga na kuswali sana na kwamba ni mke wako Peponi.”

Ameipokea pia Abu Daawuud (2283) kupitia kwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtaliki Hafswah kisha akamrejea.”

Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1975).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 11-15
  • Imechapishwa: 25/03/2024