Muhammad bin Kathiyr ametuhadithia, kutoka kwa al-Awzaa´iy, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy ´Amr as-Saybaaniy aliyeeleza kuwa Hudhayfah amesema:

“Mimi nawajua watu wa dini mbili ambao wote wako Motoni. Kundi la kwanza wanaosema kuwa imani ni kutamka ingawa mtu atazini na kuiba. Kundi lingine linasema: “Ni kitu gani swalah tano? Ni swalah mbili tu.” Akataja Maghrib, au ´Ishaa, na Fajr.

Dhamrah bin Rabiy´ah amemuhadithia Yahyaa bin Abiy ´Amr as-Saybaaniy, kutoka kwa Humayd al-Maqraaiy, kutoka kwa Hudhayfah.

Zingatia maneno haya ya Hudhayfah. Ameambatanisha Irjaa´ kwa swalah. Ibn ´Umar pia amewaeleza namna hiyo.

21 – ´Aliy bin Thaabit al-Jazariy ametuhadithia, kutoka kwa Ibn Abiy Laylaa, kutoka kwa Naafiy´, kutoka kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

“Makundi mawili hayana fungu lolote katika Uislamu: Murji-ah na Qadariyyah.”[1]

22 – ´Abdur-Rahmaan ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Salamah bin Kuhayl ambaye amesema:

“adh-Dhwahhaak, Maysarah na Abul-Bakhtariy walikubaliana juu ya kwamba ushahidi, Irjaa´ na kujitenga ni Bid´ah.”[2]

23 – Muhammad bin Kathiyr ametuhadithia, kutoka kwa al-Awzaa´iy, kutoka kwa az-Zuhriy ambaye amesema:

“Katika Uislamu hakujazuliwa Bid´ah ambayo ni tukufu zaidi kwa wenye nayo kama Irjaa´ hii.”

24 – Ismaa´iyl bin Ibraahiym ametuhadithia, kutoka kwa Mahdiy bin Maymuun, kutoka kwa al-Waliyd bin Muslim ambaye amesema:

“Aliingia fulani (Ismaa´iyl alimtaja jina lake, lakini nimeacha kufanya hivo) kwa Jundub bin ´Abdillaah al-Bajaliy na akamuuliza juu ya Aayah ndani ya Qur-aan. Akamjibu kwa maneno kama:

“Itakuwa ni aibu kwako kama wewe ni muislamu na usiondoke.”

Au alisema:

“Usiketi nami.”

25 – Ismaa´iyl bin Ibraahiym ametuhadithia, kutoka kwa Ayyuub: Sa´iyd bin Jubayr alinambia ghafla tu:

“Usiketi na fulani. Anaonelea maoni haya.”

Kuna mengi ya kusema kuhusu kuepukana na matamanio, lakini kitabu tumewakusudia watu hawa tu. Mfano wa hayo yamesemwa na Sufyaan, al-Awzaa´iy, Maalik bin Anas na waliokuja baada yao katika vigogo wa elimu na Ahl-us-Sunnah ambao walikuwa ndio taa za ardhi na viongozi wa elimu katika wakati wao. Walikuwa wakiishi ´Iraaq, Shaam na maeneo mengine. Wote waliwakosoa Ahl-ul-Bid´ah na kuona kuwa imani ni maneno na matendo.

[1] Cheni ya wapokezi ni dhaifu kwa sababu ya Ibn Abiy Laylaa ambaye jina lake ni Muhammad bin ´Abdir-Rahmaan. Hifdhi yake ilikuwa mbaya. Maneno hayo yamepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini hayakusihi. Nimefupisha maneno juu yake katika maelezo yangu ya ”al-Mishkaah” (105).

Murji-ah ni pote miongoni mwa mapote ya Uislamu. Wanaona kuwa imani haidhuriki kwa maasi kama ambavo ukafiri haunufaishi kwa utiifu. Wameitwa hivo kwa sababu ya kuona kwao kuwa Allaah ameahirisha (أرجأ) kuwaadhibu juu ya maasi, hivo ndivo imekuja katika ”an-Nihaayah”.

Qadariyyah wanapinga makadirio. Hapo zamani walikuwa wakiwakilishwa na Mu´tazilah. Hii leo mfano wao ndio wanafanya hivo.

[2] Cheni ya wapokezi wake kwa mkusanyiko uliotajwa ni Swahiyh. Wao ni katika wabora kabisa katika wanafunzi wa Maswahabah. Abul-Bakhtariy jina lake ni Sa´iyd bin Fayruuz. Alifariki mwaka wa 83. Maysarah alikuwa Ibn Ya´quub bin Jamiylah al-Kuufiy. Alikuwa mbeba bendera wa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh). adh-Dhwahhaak alikuwa Ibn Sharaahiyl al-Hamadaaniy.

Kujitenga mbali ni katika Bid´ah za khawaarij. Walimfanyia uasi ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na kujitenga naye mbali. Kisha baadaye kujitenga mbali ikawa ni katika ´Aqiydah zao wanazotambulika nazo. Mpaka wakawa wanajitenga mbali na watu wao kwa sababu ya kutofautiana nao katika suala limoja tu. Tazama ”Maqaalaat-ul-Islaamiyyiyn” (1/156-196) ya Abul-Hasan al-Ash´ariy.

Kinachodhihiri ni kwamba ushahidi ni katika Bid´ah za Murji-ah, kwa sababu wanamshuhudilia kila muumini kwamba yuko Peponi. Wanasema kuwa imani haidhuriki kwa kitendo kama ambavo shirki haunufaishi kitendo. Inawezekana pia ikawa ni katika Bid´ah za Mu´tazilah. Wametofautiana juu ya ushahidi katika maoni manne ambapo moja wapo wanasema kuwa mashahidi ndio waadilifu, ni mamoja wameuliwa katika uwanja wa vita au hawakuuliwa. Rejea maoni yao mengine katika ”Maqaalaat-ul-Islaamiyyiyn” (1/296-297) ya Abul-Hasan al-Ash´ariy.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 62-67
  • Imechapishwa: 27/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy