´Allaamah na hoja ya Uislamu Abu Ja´far al-Warraaq at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema Misri:
Huu ni ubainifu wa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa mujibu wa madhehebu ya wanachuoni wa Uislamu Abu Haniyfah an-Nu´maan bin Thaabit al-Kuufiy, Abu Yuusuf bin Ibraahiym al-Answaariy na Abu ´Abdillaah Muhammad bin al-Hasan ash-Shaybaaniy na yale wanayoamini katika misingi ya dini na kumuabudu kwayo Mola wa walimwengu – Allaah awawie radhi.
1 – Tunasema kuhusu upwekekaji wa Allaah hali ya kuwa ni wenye kuitakidi kwa tawfiyq ya Allaah ya kwamba Allaah ni mmoja asiyekuwa na mshirika.
MAELEZO
Kumkanushia Allaah mshirika hakutimii isipokuwa kwa kukanusha sampuli tatu za shirki:
1 – Shirki katika uola wa Allaah kwa njia ya kwamba mtu akaamini kuwa kuna mwingine anayeumba pamoja na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hivo ndivo wanavoamini waabudia moto. Wanaona kuwa kuna mungu mwingine wa shari asiyekuwa Allaah (Subhaanah). Himdi zote ni stahiki ya Allaah kuona aina hii katika ummah huu ni wachache. Hata hivyo Mu´tazilah hawako mbali na wao wanaosema kuwa shari inaumba mtu mwenyewe. Hayo ndio aliyokuwa akiashiria Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pale aliposema:
”Qadariyyah ni waabudia moto wa ummah huu.”[1]
2 – Shirki katika haki pekee ya Allaah ya kuabudiwa. Nayo maana yake ni mtu amwabudu mwengine asiyekuwa Allaah, kama vile Mitume na waja wema. Kwa mfano mtu akawataka uokozi na kuwaita wakati wa matatizo na mfano wake. Kwa masikitiko makubwa sampuli hii ya shirki inafanywa kwa wingi katika ummah huu. Miongoni mwa wanaobeba dhambi yake kubwa ni wale mashaykh ambao wanaisapoti shirki hii na kuiita kimakosa kwamba ni Tawassul.
3 – Shirki katika sifa za Allaah. Hapo ni pale ambapo utawasifu viumbe kwa sifa za Allaah (´Azza wa Jall). Mfano wa hilo ni kuyajua mambo yaliyofichikana. Aina hii imeenea kwa wengi katika Suufiyyah na wengineo walioathirika nao. Kwa mfano mmoja wao amesema wakati alipokuwa akimsifu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):
Hakika miongoni mwa ukarimu wako ni dunia na mali zake
na miongoni mwa ujuzi wako ni ujuzi wa Ubao na Kalamu
Kutokana na hili baadhi ya madajali wanasema eti wanamuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hii leo katika hali ya kuwa macho, na kwamba wanamuuliza yale mambo yaliyofichikana kwa wale wanaotangamana nao kwa kutaraji kuwa na mamlaka juu yao. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa anajua mambo kama hayo wakati alipokuwa hai:
قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ
“Sema: “Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa atakavyo Allaah na lau ningekuwa najua ya ghaibu, bila shaka ningelijikithirishia ya kheri na wala lisingelinigusa ovu. Mimi si chochote isipokuwa ni mwonyaji na mbashiriaji kwa watu wanaoamini.”[2]
Ni vipi basi atayajua hayo baada ya kufa kwake?
Yule anayekanusha aina tatu hizi za shirki na akaamini kuwa Allaah ni Mmoja, akamwabudu Yeye pekee na katika sifa Zake, basi huyo ndiye mpwekeshaji ambaye amekusanya zile fadhilah zote maalum zinazowahusu wapwekeshaji. Na yule anayekuwa na upungufu katika chochote katika hayo, basi huyo anaingia ndani ya maneno Yake Allaah (Ta´ala):
وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ
“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[3]
Yakumbuke haya, kwani ndio jambo muhimu zaidi katika ´Aqiydah! Hakuna ajabu kuona mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ameanza kwa jambo hilo. Anayetaka ufafanuzi zaidi basi arejee katika maelezo ya kitabu hiki na vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni wa Kiislamu, akiwemo Ibn Taymiyyah, Ibn-ul-Qayyim, Ibn ´Abdil-Wahhaab na wengineo walio na wakafuata mfumo wao:
وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا
”Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala usijaalie katika nyoyo zetu mafundo kwa wale walioamini!”[4]
[1] Nimetaja vyanzo vyake na kuikagua katika vitabu vyangu vingi na nimeashiria hilo katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (4442).
[2] 7:188
[3] 39:65
[4] 59:10
- Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
- Tarjama: Firqatunnajia.com
- Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 6-10
- Imechapishwa: 11/09/2024
Mshirikishe mwenzako:
- Click to share on Telegram (Opens in new window) Telegram
- Click to share on WhatsApp (Opens in new window) WhatsApp
- Click to print (Opens in new window) Print
- Click to email a link to a friend (Opens in new window) Email
- Click to share on Facebook (Opens in new window) Facebook
- Click to share on X (Opens in new window) X
- Click to share on Pocket (Opens in new window) Pocket