Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

2 – Hakuna kitu mfano Wake.

MAELEZO

Huu ni msingi miongoni mwa misingi ya Tawhiyd. Hakuna chochote kinachofanana na Allaah (Ta´ala), si inapokuja katika dhati, sifa wala matendo Yake. Wazushi na wapindisha maana wanatumia vibaya kanuni hii kukanusha sifa nyingi za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Kila wakati ambapo nyoyo zao zinahisi dhiki kuamini sifa yoyote miongoni mwa sifa za Allaah, basi ndio wanaingia zaidi katika kupindisha maana na kuharibu. Sambamba na hilo wanajenga hoja kwa maneno Yake Allaah (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye…”

wanafumbia macho maneno Yake:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“… Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[1]

Aayah hii imekusanya kati ya kutakasa na kuthibitisha. Yule anayetaka kusalimika katika ´Aqiydah yake basi analazimika kumtakasa Allaah (Ta´ala) kutokana na viumbe, pasi na kupindisha maana wala kukanusha, sambamba na hilo amthibitishie Allaah (´Azza wa Jall) sifa zote alizojithibitishia Mwenyewe au alizomthibitishia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bila kufananisha. Hii ndio ´Aqiydah ya Salaf na pia ndio ´Aqiydah ya mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah). Anamfuata Abu Haniyfah na maimamu wengine, kama utakavyoona inapambanuliwa katika maelezo, kwa hivyo:

فَبِهُدَاهُمُ اقْتَدِهْ

”Hivyo basi fuata kama kigezo mwongozo wao.”[2]

[1] 42:11

[2] 6:90

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 11/09/2024