Swali 01: Kulizuka mjadala juu ya vigawanyo vya maji. Miongoni mwao wako wenye kuona kuwa maji yamegawanyika mafungu mawili:

1 – Masafi.

2  – Machafu.

Wengine wakaona kuwa maji yamegawanyika mafungu matatu:

1 – Yenye kusafisha.

2 – Masafi.

3 – Machafu.

Je, usawa uko pamoja na kundi la kwanza au kundi la pili[1]?

Jibu: Maji yaliyoachiwa yamegawanyika mafungu mawili:

1 – Masafi.

2  – Machafu.

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً طَهُورًا

”Tunateremsha kutoka mawinguni maji yaliyo safi.”[2]

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ

”Wakati alipokufunikeni kwa usingizi kuwa ni amani kutoka Kwake na akakuteremshieni maji kutoka juu mbinguni ili akusafisheni kwayo na akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Maji ni masafi na hayanajisiwi na kitu.”[4]

Ameipokea Imaam Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

Makusudio yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa yale yaliyobadilika ladha, harufu au rangi yake kwa kuingiwa na kitu katika najisi. Katika hali hiyo yananajisika kwa maafikiano ya wanazuoni. Kuhusu majani, makaratasi au vitu vyenginevyo mfano wake vinavyoingia ndani ya maji basi hayanajisiki na wala hayapotezi usafi wake muda wa kuwa bado yanaitwa ´maji`.

Lakini yakibadilika jina la ´maji` kwa jina jengine ya kile kitu ambacho yamechanganyika nacho, maziwa, kahawa, chai na vyenginevyo, basi yanatoka nje ya jina ´maji` na hayaitwi tena ´maji`. Lakini yenyewe kama yenyewe ni masafi kwa kitu hichi kilichochanganyika nacho na wala hayanajisiki kwacho.

Kuhusu maji yaliyoachiwa, kama vile maji ya waridi, maji ya zabibu na maji ya komamanga, haya yanaitwa ´maji masafi` na wala hayaitwi ´maji yenye kusafisha`. Jambo la kutwahirika kutokamana na hadathi na najisi halifikiwi kwa maji haya. Kwa sababu ni maji yaliyofungamana na sio maji kwa njia ya kuachia. Hayajumuishwi na dalili za ki-Shari´ah zinazofahamisha jambo la kujitwahirisha kwa maji. Shari´ah imesifu maji yaliyoachiwa inapokuja katika jambo la kujitwahirisha. Ni kama mfano wa maji ya mvua, maji ya bahari, maji ya mto na maji ya bwawa.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/14-15).

[2] 25:48

[3] 07:11

[4] Ahmad (11406, 11409), Abu Daawuud (67) na at-Tirmidhiy (66).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 16/02/2022