02. Maji chini ya Qulatayn yanayochanganyikana na najisi

Swali 02: Maji yakipungua Qulatayn na yakachanganyikana na najisi kama vile mkojo au kinyesi – je, inaondoka ile sifa yake ya kusafisha[1]?

Jibu: Wanazuoni wametofautiana juu ya jambo hilo. Miongoni mwao wako wenye kuona maji yakiwa chini ya Qulatayn na yakapatwa na najisi, basi yananajisika kwa sababu hiyo ijapo hayakubadilika rangi, ladha au harufu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maji yakiwa Qulatayn basi hayabebi uchafu.”[2]

Imekuja katika tamko lingine:

“Maji yakiwa Qulatayn basi hayanajisiki.”

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa nne wa “as-Sunan”. Ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Khuyzamah, Ibn Hibbaan na al-Haakim.

Wamesema kuwa Hadiyth inafahamisha kwamba maji yaliyo chini ya Qulatayn yananajisika kutokana na ile najisi inayoingia ndani yake ijapo hayakubadilika.

Wanazuoni wengine wakasema kuwa ujengeaji wa ufahamu ni dhaifu.

Maoni ya sawa ni kwamba maji yaliyo chini ya Qulatayn hayanajisiki isipokuwa kwa kubadilika kama mfano wa yale maji yaliyofikia Qulatayn. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Maji ni masafi na hayanajisiwi na kitu.”[3]

Ameipokea Imaam Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kutoka kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametaja Qulatayn ili kuzindua kwamba yaliyo chini yake yanahitaji jambo la kuthibitisha, kuangaliwa na kutiliwa umuhimu. Kwa sababu yananajisika moja kwa moja kutokana na Hadiyth ya Abu Sa´iyd iliyotajwa.

Faida inayopatikana kutoka hapo ni kwamba maji kidogo sana mara nyingi yanaathirika kwa najisi. Kwa ajili hiyo inatakiwa kuyachunga na kuyalinda. Kwa ajili hiyo imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Anaporamba mbwa kwenye chombo cha mmoja wenu, basi akioshe mara saba, mojawapo kwa mchanga.”[4]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Hayo si kwa jengine isipokuwa ni kwa sababu vyombo wanavyotumia watu mara nyingi vinakuwa vidogo na hivyo vinaathirika kwa kurambwa na mbwa na kwa najisi yake ijapo ni kidogo. Kwa hivyo ikawajibika kukiosha kwa mchanga pale kinapoingiwa na najisi kwa ajili ya kuchukua tahadhari na kujiepusha na shubuha. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Achana na kile chenye kukutia shaka na kiendee kile kisichokutia shaka.”[5]

“…. yule anayeepuka vyenye shaka atakuwa amejisafisha kwenye dini yake na heshima yake.”[6]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/15-17).

[2] Ahmad (4591), Abu Daawuud (63) na an-Nasaa´iy (52).

[3] Ahmad (11406, 11409), Abu Daawuud (67) na at-Tirmidhiy (66).

[4] Muslim (636).

[5] at-Tirmidhiy (2518).

[6] al-Bukhaariy (52).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 16/02/2022