01. Kuwa na ujuzi kwa Allaah, Mtume Wake na dini ya Kiislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah Akurehemu – ya kwamba ni wajibu juu yetu kujifunza masuala mane:

Suala la kwanza: Ujuzi, nao ni ujuzi wa kumjua Allaah, ujuzi wa kumjua Mtume Wake na ujuzi wa kuijua Dini ya Kiislamu kwa dalili.

Suala la pili: Kuifanyia kazi.

Suala la tatu: Kuilingania.

Suala la nne: Kusubiri juu ya maudhi yatakayompata mtu ndani yake. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.” (al-´Aswr 103 : 01-03)

ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lau Allaah Asingeliteremsha hoja yoyote kwa viumbe Wake isipokuwa Suurah hii, basi ingeliwatosheleza.”

al-Bukhaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.” (Muhammad 47 : 19)

Akawa ameanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo.”

MAELEZO

Waumini wote wanaume kwa wanawake, wadogo kwa wakubwa, ni wajibu kujifunza masuala haya mane.

Suala la kwanza ni ujuzi wa kumtambua Allaah. Ni lazima kwa mtu kujifunza na kuwa na uelewa ili awe juu ya ubainifu. Ni lazima kwake kuitambua dini ya Allaah ambayo ameumbwa kwa ajili yake. Ujuzi huu ni kumtambua Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na dini ya Kiislamu kwa dalili.

Kitu cha kwanza kabisa mja anatakiwa kujifunza kuhusu Mola wake. Anatakiwa kutambua kuwa Mola wake ni Muumbaji aliyemuumba na kumruzuku. Akamtunuku neema. Yeye ndiye kawaumba walio kabla yake na ndiye atayewaumba walio baada yake. Yeye ndiye Mola wa walimwengu. Yeye ndiye Mungu wa haki. Hakuna mwingine anayestahiki kuabudiwa asiyekuwa Yeye; si Malaika walio karibu, wala Mitume waliotumwa, wala majini, wala masanamu – na visivyokuwa hivyo. ´Ibaadah zote ni haki ya Allaah peke yake. Yeye pekee (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye anayestahiki kuabudiwa.

Mola wa walimwengu peke yake ndiye anastahiki kuabudiwa. Yeye ndiye Mola wako, Muumbaji wako na Mungu wa haki (Subhanaahu wa Ta´ala). Kuwa na ujuzi kumtambua Mola wako, Mtume wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na dini yako kwa dalili. Mnukuu Allaah na Mtume wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Usizungumze kwa maoni wala visa vya fulani. Zungumza kwa dalili za Aayah na Hadiyth. Ndio Uislamu ambao umeamrishwa kuamini na kuutendea kazi.

Ndio dini ya Uislamu ambayo ni kumuabudu Allaah. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wanaadamu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

´Ibaadah hii ndio Uislamu; kumtii Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusimamisha maamrisho ya Allaah na kuacha makatazo Yake. Watu wameumbwa kwa ajili ya hili. Allaah amewaamrisha watu nayo pale aliposema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu.” (02:21)

Muabuduni kwa kutekeleza maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Jisalimisheni Kwake na mumuabudu Yeye peke yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Katika ujuzi huo kunaingia vilevile kuwa na utambuzi kuhusu Mtume wako (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib al-Haashimiy al-Qurashiy al-Makkiy na baadae al-Madaniy. Unatakiwa kutambua kuwa yeye ndiye Mtume wako na kwamba Allaah amemtuma kwa dini ya haki ili akufunze na kukuelekeza. Unatakiwa kuamini kuwa yeye ni Mtume wa Allaah wa kweli na kwamba Allaah amemtuma kwa walimwengu majini na watu. Ni wajibu kumfuata na kuiga mfumo wake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 06-07
  • Imechapishwa: 15/10/2016