01. Kupambana katika kumi la mwisho la Ramadhaan

01 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalipokuwa yanaingia yale masiku kumi ya mwisho basi anauhuisha usiku wake, anawaamsha ahli zake, anajipinda na hukaza vizuri kikoi chake.”

Kuna maafikiano juu yake.

Imekuja katika upokezi wa Muslim:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika masiku kumi ya mwisho ambavyo hajitahidi katika masiku mengine.”[1]

Hadiyth zinafahamisha kuwa zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan zina sifa maalum kuliko masiku mengine kwa kuzidisha utiifu, ´ibaadah, swalah, Dhikr na kisomo cha Qur-aan.

Mama wa waumini, mama yetu ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amemsifu Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sifa nne:

1 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… anauhuisha usiku wake… “

Bi maana anakesha ambapo anauhuisha kwa utiifu na anajiandaa nafsi yake kukesha ndani yake. Kwa sababu usingizi ni ndugu yake kifo. Maana yake ni kwamba anahuisha usiku kwa kusimama na kujikurubisha kwa Allaah, Mola wa walimwengu. Kuhusu yaliyopokelewa juu ya makatazo ya kusimama usiku mzima kwa ajili ya kuswali katika Hadiyth ya ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa)[2], kunafasiriwa kuhusu ambaye atadumu kufanya hivo katika nyusiku zote za mwaka[3]. Kuna uwezekano vilevile maana yake amehuisha sehemu kubwa ya usiku. Kinachotilia nguvu hayo ni maneno yake ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Sijawahi kumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisimama usiku mpaka asubuhi.”[4]

2 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… anawaamsha ahli zake… “

Bi maana wake zake watwahirifu ambao ni mama wa waumini (Radhiya Allaahu ´anhunna) ili wapate kushirikiana naye kheri, Dhirk na ´ibaadah ndani ya kipindi hichi kilichobarikiwa.

3 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… anajipinda… “

Bi maana anajitahidi katika ´ibaadah akiongezea juu ya ´ibaadah zake katika zile siku ishirini za mwanzo. Hilo ni kwa sababu usiku wa Qadar unakuwa katika hizi siku za mwisho.

4 – Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… hukaza vizuri kikoi chake… “

Bi maana kufanya bidii katika ´ibaadah. Maoni mengine yamesema kuwa anajitenga na wanawake. Hili ndio dhahiri zaidi kwa kuungana kwake na ya kabla yake. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliikaa I´tikaaf katika zile siku kumi za mwisho na mwenye kukaa I´tikaaf amekatazwa kutokana na wanawake.

[1] al-Bukhaariy (2024) na Muslim (1174).

[2] al-Bukhaariy (1974) na Muslim (1159).

[3] Majmuu´-ul-Fatawaa (22/308).

[4] Muslim (746), (141) na pia tazama ”Latwaaif-ul-Maa´rif” (216-217).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtaswar Ahaadiyth-is-Swiyaam, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 25/02/2023