01. Kufunga Ramadhaan kunawajibika kwa mambo gani?

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Ni lazima kufunga Ramadhaan kwa moja kati ya mambo mawili:

1 – Kuonekana kwa mwezi mwandamo wa Ramadhaan.

2 – Kukamilisha Sha´baan siku thelathini.

Vilevile ni lazima kufungua Ramadhaan kwa moja kati ya mambo mawili:

1 – Kuonekana mwezi mwandamo wa Shawwaal. Ikithibiti kuonekana mwezi mwandamo wa Shawwaal kwa ushahidi wa wanamme wawili waadilifu.

2 – Kukamilisha Ramadhaan siku thelathini.

Dalili juu ya hayo ni nyingi ndani ya Sunnah Takasifu. Miongoni mwazo ni yale yaliyothibiti katika ”as-Swahiyh” ya al-Bukhaariy kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitaja Ramadhaan kisha akasema:

”Msifunge mpaka muone mwezi mwandamo na wala msifungue mpaka muuone. Mkifunikwa na mwingu basi ukadirieni.”[1]

 ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mwezi ni nyusiku ishirini na tisa. Kwa hivyo msifunge mpaka muuone. Mkifunikwa na mwingu, basi kamilisheni idadi ya thelathini.”[2]

Imepokelewa katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Fungeni kwa kuuona na mfungue kwa kuuona. Mkifunikwa na mawingu, basi kamilisheni idadi ya thelathini.”[3]

Kikosi cha wanazuoni wengi wanaona makusudio ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… basi ukadirieni.”

tazameni kuanzia mwanzo wa mwezi, hesabuni vyema kukamilika kwa siku thelathini. Kitu kinachotia nguvu tafsiri hii ni mapokezi mengine yanayosema wazi kilichokusudiwa. Kwa mfano maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth ya Ibn ´Umar iliyotangulia:

“…basi kamilisheni idadi ya thelathini.”

Vilevile Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ilioko kwa Muslim:

“Mkifunikwa na mwingu basi kadirieni thelathini.”

Pia katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ilioko kwa Muslim:

“Mawingu yakikufunikeni ndani ya mwezi, basi hesabuni thelathini.”[4]

Kadhalika katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Mkifunikwa na mawingu, basi kamilisheni idadi ya Sha´baan thelathini.”

Kitu bora kinachoweza kuifasiri Hadiyth ni Hadiyth nyingine. Kwa hivyo watu wasifunge isipokuwa kwa kuona mwezi mwandamo au kwa kukamilisha idadi ya mwezi siku thelathini. Ni mamoja mwezi ni wa Sha´baan au Ramadhaan. Kinachotilia nguvu maana na tafsiri hii ni Hadiyth zilizopokelewa kuhusu kufunga siku ya shaka. Moja wapo ni ile aliyopokea Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Asiitangulizie mmoja wenu Ramadhaan kwa kufunga siku moja au siku mbili; isipokuwa ikiwa ni mtu aliyezowea kufunga swawm yake basi afunge siku hiyo.”[5]

Vilevile Hadiyth ya ´Ammaar (Rdhiya Allaahu ´anh) ilioko kwa al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu hali ya kuashiria kuwa imethibiti:

“Yeyote mwenye kufunga siku ya shaka, basi hakika amemuasi Abul-Qaasim.”[6]

Imepokelewa katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwezi ni namna hii na namna hii”akakunja kidole gumba mara ya tatu”.”[7]

Maana ya Hadiyth ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwezi ni namna hii… “

Bi maana alikutanisha vidole vya mikono yake ambapo ikawa kumi. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na namna hii.”

Akakutanisha vidole vya mikono yake ambapo ikawa kumi kwa mara ya pili. Hapo inakuwa siku ishirini. Kisha akakutanisha vidole vyake kumi kwa mara ya tatu kisha akakunja kidole gumba na hivyo inakuwa siku tisa pamoja na zile ishirini zilizotangulia na jumla mwezi inakuwa ishirini na tisa. Kwa maana nyingine hili ni lenye uhakika. Wakati mwingine inaweza kukamilika na hivyo ikawa siku thelathini.

Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim waliopokea kupitia kwa Ibn ´Umar  (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika sisi ni ummah tusiokuwa wasomi; hatuandiki wala hatuhesabu. Mwezi ni namna hii na namna hii.” Bi maana mara inakuwa siku ishirini na tisa na mara nyingine inakuwa siku thelathini[8].

Hadiyh hii ni dalili juu ya ubatilifu wa kutegemea hesabu juu ya kuanza na kumalizika kwa mwezi. Hakika hapana vyenginevyo kinachotegemewa ni kuonekana mwezi mwandamo au kukamilisha idadi ya mwezi siku thelathini. Hadiyth imetueleza jamii hii ya kiislamu kwa sifa ya kuzingatia wingi; ya kwamba si katika kazi zao kuandika na kuhesabu wakati wa kuanza na kumalizika kwa mwezi ingawa wanaandika na wanahesabu katika mambo mengine kama vile mambo ya biashara na mengineyo. Kinachokusudiwa ni kwamba hawategemei hesabu. Hakika si vyenginevyo wanachotegemea ni mwezi mwandamo katika hukumu mbalimbali. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefungamanisha hukumu na mwezi mwandamo na si kwa kuhesabu. Mwezi mwandamo ni kitu kinachotambulika na mtu wa kawaida, mjinga na msomi, jambo ambalo linafahamisha wepesi wa Shari´ah na himdi zote njema anastahiki Allaah kwa yale aliyoyafanya wepesi na sahali. Anayo hekima kamili juu ya yale anayowawekea Shari´ah waja kutokana na yale manufaa na huruma, anayoyatambua (Subhaanah) juu yao. Hakika Yeye ni mwingi wa hekima, mjuzi wa kila kitu.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] al-Bukhaariy (1906) na Muslim (1080).

[2] al-Bukhaariy (1907).

[3] al-Bukhaariy (1909).

[4] Muslim (1081).

[5] al-Bukhaariy (1914) na Muslim (1082).

[6] al-Bukhaariy (03/27).

[7] al-Bukhaariy (1980).

[8] al-Bukhaariy (1913) na Muslim (1080).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 09-12
  • Imechapishwa: 09/04/2023