01. Hukumu ya Tarawiyh na idadi ya Rak´ah zake

Aliulizwa muheshimiwa Shaykh al-´Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) swali lifuatalo: Ni ipi hukumu ya swalah ya Tarawiyh? Ni ipi Sunnah juu ya idadi ya Rak´ah zake?

Akajibu ifuatavyo: Swalah ya Tarawiyh ni Sunnah aliyoisunisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya ummah wake. Alisimama kuswali na Maswahabah zake nyusiku tatu lakini baadaye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaacha kufanya hivo kwa kuchelea isije kufaradhishwa juu yao. Kisha baada ya hapo waislamu wakabaki katika hali hiyo katika zama za Abu Bakr na katika uongozi wa ´Umar. Baada ya hapo kiongozi wa waumini ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akawakusanya kwa Tamiym-ud-Daariy na Ubay bin Ka´b. Wakawa ni wenye kuswali kwa mkusanyiko mpaka hii leo na himdi zote anastahiki Allaah. Kwa hivyo imependekezwa katika Ramadhaan.

Kuhusu idadi ya Rak´ah zake ni Rak´ah kumi na moja au Rak´ah kumi na mbili. Hii ndio Sunnah katika jambo hilo. Lakini endapo mtu atazidisha juu ya hizo hakuna neno wala ubaya. Kwa sababu kumepokelewa juu ya hilo kutoka kwa Salaf aina mbalimbali katika kuongeza na kupunguza. Hakuna baadhi ambao waliwakemea wengine. Kwa hivyo asikaripiwe yule ambaye atazidisha ijapo bora ni kwa yule ambaye atakomeka na ile idadi iliopokelewa. Isitoshe Sunnah pia imejulisha kwamba hakuna ubaya kuzidisha. al-Bukhaariy na wengineo wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar ambaye amesimulia kuwa kuna mtu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu swalah ya usiku ambapo akajibu:

“Ni [Rak´ah] mbilimbili. Atakapochelea mmoja wenu Subh basi ataswali [Rak´ah] moja ili kuwitirisha yale aliyoswali.”[1]

Hakuweka kikomo cha idadi maalum (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambacho mtu atafupika kwacho. Lakini lililo muhimu katika swalah ya Tarawiyh ni unyenyekevu na utulivu katika Rukuu´, Sujuud na wakati wa kuinuka kutoka katika Rukuu´ na Sujuud. Mtu asifanye ile haraka ya spidi inayofanywa na baadhi ya watu ambayo inawakosesha waswaliji kufanya yale mambo yaliyosuniwa. Bali huenda spidi yake ikawakosesha kufanya yale mambo yaliyowajibishwa kwa ajili ya kupupia awe wa kwanza kutoka kwenye misikiti ili watu wapate kukusanyika kwake kwa wingi zaidi. Kitendo hichi ni chenye kwenda kinyume na yale yaliyowekwa katika Shari´ah.

Ni lazima kwa imamu kumcha Allaah juu ya wale walioko nyuma yake na asirefushe urefushaji ambao unawatia uzito unaotoka nje ya Sunnah kama ambavo pia asiwepesishe uwepesi ambao unaharibu yale mambo ya wajibu au yaliyosuniwa kwa wale walioko nyuma yake. Kwa ajili hii wanachuoni wamesema:

“Imechukizwa kwa imamu kufanya haraka itakayowakosesha waswaliji kufanya yale yaliyopendekezwa.”

Tusemeje kwa wale wanaofanya haraka inayowakosesha waswaliji kufanya yale ambayo ni ya wajibu? Hakika haraka kama hii ni ya haramu juu ya imamu huyu. Tunamuomba Allaah atupe sisi na ndugu zetu msimamo na usalama.

[1] al-Bukhaariy (990) na Muslim (1695).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 05-06
  • Imechapishwa: 02/04/2022