01. Hadiyth “Nimeshajua kuwa unapenda kuswali pamoja nami… “

340 – Umm Humayd, mwanamke wa Abu Humayd (Radhiya Allaahu ´anhumaa), ameeleza:

“Alienda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mimi napenda kuswali pamoja nawe.” Akasema:

قد علمتُ أنَّكِ تُحبّين الصلاةَ معي، وصلاتُكِ في بيتكِ خيرٌ من صلاتِكِ في حُجرتِكِ، وصلاتُكِ في حُجرتِكَ خيرٌ من صلاتِكِ في دارِكِ، وصلاتُكِ في دارِكِ خيرٌ من صلاتِكِ في مسجدِ قومِكِ، وصلاتُكَ في مسجدِ قومِكِ خيرٌ من صلاتِكِ في مسجدي

“Nimeshajua kuwa unapenda kuswali pamoja nami, lakini swalah yako katika pembe yako ni bora kuliko swalah yako katika chumba chako, na swalah yako katika chumba  chako ni bora kuliko swalah yako katika nyumba yako, na swalah yako katika nyumba yako ni bora kuliko swalah yako katika msikiti wako wa karibu, na swalah yako katika msikiti ulio karibu ni bora kuliko swalah yako katika msikiti wangu.” Akaamrisha ajengewe msikiti sehemu iliyojitenga na yenye giza zaidi katika nyumba yake ambapo alikuwa anaswali maeneo hapo mpaka alipokutana na Allaah (´Azza wa Jall).”[1]

Ameipokea Ahmad, Ibn Khuzaymah katika ”as-Swahiyh” na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake. Ibn Khuzaymah ameiwekea kichwa cha khabari kinachosema:

“Mwanamke kupendelea kuswali chumbani kwake juu ya kuswali nyumbani kwake na kuswali katika msikiti ulio karibu naye juu ya kuswali katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ijapo kuswali katika msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni sawa na kuswali swalah elfu moja katika misikiti mingine. Dalili ya hilo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuswali katika msikiti huu ni bora kuliko swalah elfu moja katika misikiti mingine.”

Amewakusudia wanaumme na si wanawake.”[2]

[1] Nzuri kupitia zingine.

[2] Ni jambo linahitaji kuangaliwa vyema na kwa ajili hiyo nikaliwekea maelezo katika “as-Swahiyhah” (03/94) na kusema:

“Hadiyth inawakusanya wanawake pia. Haipingani na kwamba bora ni kuswali kwao nyumbani. Kadhalika mwanaume anaposwali swalah ya kujitolea katika msikiti wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi anapata fadhilah zilizotajwa, ingawa ni bora kuiswali nyumbani. Zingatia jambo hilo!”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Adhwiym bin ´Abdil-Qawiy al-Mundhiriy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/258)
  • Imechapishwa: 16/12/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy