01. Aayah za Qur-aan na Hadiyth zinazokemea Bid´ah

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote na wale wote watakaofuata mwenendo wao.

Amma ba´d:

Kumeulizwa maswali mengi kuhusu hukumu ya kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kusimama katikati yake, kumtolea salamu na mengineyo yanayofanyika katika mazazi.

Jibu ni kwamba: haijuzu kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala ya mwengine. Kwa sababu kufanya hivo ni Bid´ah iliyozuliwa ndani ya dini. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupatapo kufanya hivo, makhaliyfah zake waongofu wala wengineo katika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wala wale waliofuatia baada ya hapo katika zile karne bora – ilihali wao ndio watambuzi zaidi wa Sunnah na wenye mapenzi kamilifu zaidi kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Shari´ah yake kuwashinda wale waliokuja baada yao. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

”Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa.”[1]

Bi maana atarudishiwa mwenyewe.

Amesema katika Hadiyth nyingine:

”Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu wenye kuongoza baada yangu. Shikamaneni nazo na ziumeni kwa magego yenu. Tahadharini na mambo yaliyozuliwa. Kwani hakika kila kilichozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotofu.”[2]

Katika Hadiyth hizi mbili kuna matahadharisho makali ya kuzua Bid´ah na kuifanya kazi.

Allaah (Subhaanah) amesema katika Kitabu Chake kinachobainisha:

وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا

”Kile alichokupeni Mtume basi kichukueni na kile alichokukatazeni basi kiacheni.”[3]

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokwenda kinyume amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[4]

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[5]

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia mwanzoni ambao ni Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[6]

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

 “Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.”[7]

Zipo Aayah nyingi zenye maana kama hii.

[1] al-Bukhaariy (2550) na Muslim (1718).

[2] Abu Daawuud (4607) na at-Tirmidhiy (2676).

[3] 59:07

[4] 24:63

[5] 33:21

[6] 09:100

[7] 05:03

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr minal-Bid´ah, uk. 05-07
  • Imechapishwa: 11/01/2022