00. Sababu mbili kuu za kutunga kitabu “Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah”

Himdi zote ni stahiki ya Allaah.  Tunamhimidi Yeye, tunamtaka msaada na msamaha. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpotosha, na yule aliyepotoshwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Enyi walioamini! Mcheni Allaah ukweli wa kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.”[1]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا

“Enyi watu! Mcheni Mola wenu ambaye amekuumbeni kutokana na nafsi moja na akaumba kutoka humo mke wake na akaeneza kutoka hao wawili wanamme wengi na wanawake na mcheni Allaah ambaye Kwake mnaombana na jamaa. Hakika Allaah amekuwa juu yenu ni Mwenye kuchunga.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا

“Enyi mlaomini! Mcheni Allaah na semeni kauli ya kweli [ya sawasawa]. Atakutengenezeeni ‘amali zenu na Kukusameheeni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Mtume Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu.”[3]

Hakika mazungumzo ya kweli kabisa ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora kabisa ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakika uovu wa mambo ni yale yaliyozuliwa, kila kilichozuliwa ni Bid´ah, kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.

Amma ba´d:

Da´wah ya Salafiyyah imesimama juu ya baadhi ya misingi. Misingi hiyo inaiweka wazi kutokamana na mapote mengine yaliyopinda kutoka katika njia ilionyooka.

Kuna mambo mawili yaliyo wazi yaliyonifanya kuikusanya:

1- Kutokana na yale niliyoyaona mimi na wengine ambavo baadhi ya makundi ya Kiislamu ya kivyamakivyama namna yalivyokuwa mbali na mfumo wa Salaf kwa jina hili lililo wazi tukufu au yale yanayopelekea katika maana yake katika kujinasibisha na as-Salaf as-Swaalih (Radhiya Allaahu ´anhum) ambao Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu yao:

“Karne bora ni ile yangu, kisha ile itakayofuatia, kisha ile itakayofuatia, kisha ile itakayofuatia.”[4]

Matokeo yake makundi haya ya kivyamavyama yakaanza kutoa vitabu vyao kwa kutumia jina la Salaf na Ahl-us-Sunnah. Kwa kitendo hichi wanaweka sumu ndani ya asali. Wamejiweka nyuma ya jina hili kwa lengo la kuwatatiza na kuwapotosha watu. Lakini hata hivyo ukitazama vitabu hivi utaona kuna mambo mengi ambayo yako mbali kabisa na mfumo wa Salaf na kunusuru kwao madhehebu ya waliokuja nyuma na mapote potofu kama mfano wa Khawaarij, Mu´tazilah na Suufiyyah.

2- Makundi hayo au baadhi yake wamewashikilia baadhi ya Ahl-us-Sunnah al-Jamaa´ah kwa sababu tu ya kutekeleza lengo fulani ambalo linaweza kufikiwa kupitia njia ya mtu huyu ambaye wamemshikilia. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba mtu huyo utamkuta amejitenga mbali kabisa na watu hao. Ili maneno yangu yapate kuwa wazi zaidi, basi mimi hivi sasa nasema: kundi la al-Ikhwaan al-Muslimuun wameshikilia juhudi za Shaykh Muhammad bin Ibraahiym (Rahimahu Allaah) kwa yale wanayoita kuwa ni Haakimiyyah. Wakadhihirisha juhudi za imamu huyu katika masuala haya kwa kufikiria kwao kwamba ndani ya maneno yake kuna yanayosapoti batili yao waliyomo kama mfano wa kuikufurisha nchi na baada ya hapo kufanya uasi dhidi yake. Naapa kwa Allaah kwamba wamemsemea na kumzulia uongo. Msimamo wake juu ya nchi hii uko wazi pasi na vumbi juu yake. Amezungumza maneno mazuri katika kitabu kwa jina “Naswiyhat-ul-Muhimmah fiy Thalaathi Qadhwaayaa.” Humo ametaja msimamo wake kwa watawala na ameweka wazi kwamba ni lazima kuwatii katika yasiyokuwa maasi.

Maneno haya aliyotaja Shaykh katika kitabu hicho na mfano wake ni miongoni mwa msingi wa maudhui ya juhudi za Shaykh katika Haakimiyyah. Lakini watu hawa ni mfano wa wale walioweka vidole vyao juu ya Aayah za Tawraat zilizowataja wazinzi zinazobainisha ulazima wa kuwapiga mawe. Lakini hata hivo wakazificha[5]. Tunamuomba Allaah usalama na afya. Licha ya kuwa istilahi ya Haakimiyyah yenyewe imetiwa dosari. Imekosolewa na waandishi na wafikiriaji wengi. Dr. Muhammad ´Imaarah amesema:

“Ni nembo iliyochomekwa juu ya kazi zetu za kale na ijtihadi zetu za sasa.”

Baadhi ya waandishi, kama mfano wa Muhamamd Sa´iyd al-´Ashmaawiy, Ahmad Kamaal na Haafidhw Diyaab, wameonelea kuwa nembo hii ndio ileile ya Khawaarij waliyoinyanyua kipindi cha ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) inayosema:

“Hakuna hukumu isipokuwa ya Allaah.”

Kwa hiyo kama nilivyotangulia kusema wakati nilipoona kitendo hichi kibaya kutoka kwa makundi haya kinawaathiri baadhi ya vijana wetu na wakadanganyika na nembo mfano wa hizi, ndio nikapendelea kutaja misingi ya Da´wah ya Salafiyyah ambayo itawapambanua watu wa haki na wengineo.

[1] 33:102

[2] 04:01

[3] 33:70-71

[4] al-Bukhaariy (2469) na Muslim (6533).

[5] al-Bukhaariy (6841) (1699).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 17-21
  • Imechapishwa: 13/07/2020