Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amekadiria na akaongoza na akamuumba mume na mke kutokana na tone la manii linapomiminwa. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika – ni Zake sifa njema zote Aakhirah na duniani. Pia nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake ambaye alisafirishwa wakati wa usiku kwenda juu mbinguni ambapo akaona alama kubwa za Mola Wake – swalah na amani nyingi na za milele zimwendee yeye, familia yake na Maswahabah zake watukufu.

Amma ba´d;

Wakati ilipokuwa mwanamke wa Kiislamu ana nafasi yake katika Uislamu na amekabidhiwa kazi nyingi muhimu. Isitoshe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwapa wanawake miongozo maalum na akaacha anausia juu yao katika Khutbah yake ´Arafah. Mambo haya yanajulisha kuwatilia umuhimu katika kila zama na khaswakhaswa katika zama hizi ambapo mwanamke wa Kiislamu anapigwa vita kwa njia maalum kwa ajili ya kumnyang´anya heshima yake na kumshusha kutoka katika nafasi yake. Kwa hivyo ikalazimika kumjulisha khatari hiyo na kumuelekeza njia itakayomfanya kuokoka. Nataraji kitabu hiki kitakuwa ni ishara ya njia hii kutokana na baadhi ya zile hukumu maalum zitazotajwa ndani yake. Ni mchango mdogo, lakini ni juhudi za mwenye kujaribu kupunguza. Nataraji pia kuwa Allaah atanufaisha kwa kiwango chake. Hii ni hatua ya kwanza katika njia hii ambayo natumai itafuatiwa na hatua za jumla na zilizoenea zaidi katika ambayo ni mazuri na kamili zaidi.

Nilichokiwasilisha katika harakaharaka hii kimekusanya vipengele vifuatayo:

1 – Hukumu zenye kuenea.

2 – Kubainisha hukumu zinazohusu kuupamba mwili wa mwanamke.

3 – Hukumu kuhusu hedhi, damu ya ugonjwa na damu ya uzazi.

4 – Hukumu zinazohusu mavazi na Hijaab.

5 – Kubainisha hukumu zinazohusu swalah ya mwanamke.

6 – Hukumu zinazomuhusu mwanamke katika mlango wa jeneza.

7 – Hukumu zinazomuhusu mwanamke katika mlango wa swawm.

8 – Hukumu zinazomuhusu mwanamke katika Hajj na ´Umrah.

9 – Hukumu zinazowahusu wanandoa.

10 – Kubainisha hukumu zinazohifadhi utukufu wa mwanamke na kulinda heshima yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 05-06
  • Imechapishwa: 16/09/2022