Uislamu sio dini ya kumwaga damu, lakini ni dini ya Jihaad

Ibn ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Haibatilishwi kwa dhuluma ya mwenye kudhulumu wala uadilifu wa mwenye kufanya uadilifu.”

Bi maana Jihaad haibatilishwa kwa dhuluma za mwenye kufanya dhuluma. Hakuna yeyote anafaa kuzuia Jihaad na kusema kuwa hakuna Jihaad na kwamba Uislamu sio dini ya Jihaad na vita. Hii leo yanasemwa haya. Wanasema kuwa Uislamu sio dini ya Jihaad wala dini ya kumwaga damu. Ni kweli kwamba Uislamu sio dini ya kumwaga damu. Lakini ni dini ya Jihaad; si kwa sababu ya kumwaga damu, bali ni kwa sababu ya manufaa ya binadamu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema juu ya haki ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ

“Hatukukutuma isipokuwa ni rehema kwa walimwengu.”[1]

Katika huruma ya Allaah juu ya walimwengu ni Yeye kuweka Shari´ah ya Jihaad ili kuwaokoa kutoka katika giza na kuwapeleka katika nuru, kutoka katika ukafiri kwenda katika imani. Sisi hatuwapigi vita makafiri kwa ajili ya tamaa juu ya mali zao, damu zao au miji yao. Tunawapiga vita kwa ajili ya kueneza Uislamu na kwa manufaa yao. Kuingia kwao ndani ya Uislamu ni kwa manufaa yao wao wenyewe ili wafe juu ya Uislamu na waingie Peponi. Lakini wakiachwa na wakafa juu ya ukafiri wataingia Motoni. Kwa hiyo Jihaad manufaa zaidi yanawarudilia makafiri wenyewe. Kwa sababu ni kuwaokoa kutoka katika ukafiri, Moto, ujinga na upotevu. Mnaona matunda ya Jihaad mashariki na magharibi na ni kheri ngapi imezalisha, elimu kiasi gani imeeneza, kueneza Tawhiyd na kueneza Uislamu na kutokomeza dhuluma.

[1] 21:107

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydatu al-Imaam-il-Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 126-127
  • Imechapishwa: 31/01/2020