Ndio maana al-Albaaniy hakufurishi mabunge katika miji ya Kiislamu

Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh: Kwa mnasaba wa mada hii iliyokuja katika mkutano huo nilitaja maneno ya Allaah (´Azza wa Jall):

إِذْ قَالُوا لِقَوْمِهِمْ إِنَّا بُرَآءُ مِنكُمْ وَمِمَّا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ كَفَرْنَا بِكُمْ وَبَدَا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُ مُ الْعَدَاوَةُ وَالْبَغْضَاءُ أَبَدًا حَتَّىٰ تُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ

”Walipowaambia watu wao: “Hakika sisi tumejitenga mbali nanyi na yale yote mnayoyaabudu badala ya Allaah. Tunakukanusheni na umedhihirika baina yetu na baina yenu uadui na bughudha ya milele mpaka mumuamini Allaah pekee.”[1]

Ni dalili kwamba uadui na chuki ni vyenye kuendelea mpaka pale itapopatikana imani. Kukipatikana kumwamini Allaah na ikatokomea shirki, ni mamoja katika Shari´ah au ´ibaadah, basi hapo ndipo kutapatikana urafiki na mapenzi. Aayah hii ni dalili ya wazi inayoonyesha kwamba haifai kuingia bungeni au kuchukulia wepesi jambo hilo namna hiyo. Wanaketi pambizoni na wakomunisti, wakanamungu, makafiri, washirikina, waabudia makaburi au wengineo kana kwamba ni ndugu. Je, utumiaji wa dalili ni wa sawa?

Imaam al-Albaaniy: Sionelei hivo. Hapana shaka yoyote kwamba ndani ya Aayah kuna uhusiano wa wazi kati ya muislamu na washirikina. Sisi hii leo hatuwezi kuwahukumu wale wenye kukaa ndani ya bunge katika miji ya Kiislamu kwamba ni washirikina. Nafikiria kwamba unakubali, au angalau kwa uchache unajua, upambanuzi wa kielimu ambao mara nyingi unatajwa na Ibn Taymiyyah na Ibn Qayyim-il-Jawziyyah; kwamba ukafiri umegawanyika aina mbili: ukafiri wa kiimani na ukafiri wa kimatendo. Ambaye anatumbukia katika kufuru ya kimatendo haijuzu kutangamana naye kama ambaye ametumbukia katika kufuru ya kiimani. Je, unaonelea upambanuzi huu?

Shaykh Swaalih bin ´Abdil-´Aziyz Aalush-Shaykh: Hapana shaka juu ya hilo inapokuja kwa mtu mmoja mmoja. Lakini hali ya hivi sasa ni kwamba nchi zinasapoti shirki, kuitetea bali kupambana na yule anayekemea shirki.

Imaam al-Albaaniy: Hilo pia naonelea kuwa linahitajia kutazamwa vizuri. Wakati unapozungumza nchi au serikali, wewe mwenyewe unajua kuwa serikali zina watu mbalimbali. Pindi tunapotazama watu hawa mbalimbali tunazingatia wale wengi wao. Je, tunawazingatia kama waislamu wa dhahiri? Au tunawazingatia kama makafiri na washirikina? Ikiwa chaguo la kwanza litakuwa na nguvu zaidi juu ya chaguo la pili, basi tutasema kuwa ni waislamu na kwamba wanapaswa kutaamiliwa kama waislamu. Vinginevyo itakuwa ni hilo chaguo la pili. Kwa ajili hiyo kutofautisha kati ya watu na serikali ni katika upande wa kinadharia tu na si wa uhalisia. Kwa sababu nchi au serikali ziko na watu; wafalme, mawaziri na manaibu waziri. Ima tukawahukumu watu hawa kwamba ni waislamu, pasi na kujali namna walivyo, au tukawahukumu kuwa ni makafiri. Hatuwezi kusema bunge lililo na mfalme anayeswali na kufunga, mawaziri wanaoswali na kufunga na manaibu waziri wanaoswali na kufunga ni kama mfano wa watu wa Ibraahiym (´alayhis-Salaam) ambao alijitenga nao mbali katika ile Aayah ilio wazi kabisa. Hapana tofauti yoyote kwamba inatakiwa kujitenga mbali na shirki na washirikina. Lakini maudhui muhimu ni sisi kuwa wasahihi katika jambo hili; tunajitenga nao mbali kwa sababu ni washirikina au kwa sababu ni waislamu wapotofu?

[1] 60:04

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (1003) Tarehe: 1410-01-19/1989-08-21
  • Imechapishwa: 01/09/2021