1 – Ni wajibu kwa mtu kukubali zawadi pindi anapopewa. Haifai kuirudisha nyuma. Kisha alipe kwayo akiweza na ashukuru kwa ajili yake. Napendekeza ndugu wapeane zawadi kati yao. Zawadi inapelekea katika mapenzi na kuondosha vifundo.

2 – ´Abdul-Malik bin Rifaa´ah al-Fahmiy amesema:

“Zawadi ni uchawi wa dhahiri.”

3 – Abaan amesema:

“al-Hasan bin ´Amaarah alifikiwa na khabari kwamba al-A´mash anamsema vibaya. Hivyo akamtumia nguo. Baada ya hapo al-A´mash akawa anamsifu. Watu wakamwambia: “Ni vipi ulikuwa ukimsema vibaya kisha baadaye unamsifu?” Akasema: “Khaythamah amenihadithia kwamba Ibn Mas´uud amesema: “Mioyo imeumbwa kwa maumbile ya kumpenda yule mwenye kumfanyia wema na kumchukia yule mwenye kumfanyia vibaya.”

4 – Ibn Siyriyn amesema:

“Walikuwa wakipeana zawadi kwenye sahani.”

5 – Ni wajibu kwa mwenye busara kutumia vitu vinavyoendana na wakati huo na kuridhia makadirio. Asiridhie jengine zaidi ya kile alichoruzukiwa. Kama yuko na kitu kibaya basi asiache kukitoa kwa sababu tu anakidharau. Kwa sababu uchache kabisa wa hatua hiyo ni ubakhili na uzuizi. Yule anayekidharau kitu hakitoi.

6 – al-Asmaa´iy amesema:

“Tuliingia nyumbani kwa Kahmas akatupa tende ishirini na tano ambazo hazikuwa tosa, nyekundu. Akasema: “Hii ndio jitihada ya ndugu yenu na Allaah ndiye mwenye kutakwa msaada.”

7 – Maymuun amesema:

“Yule anayetaka kufanya urafiki na ndugu bila kuwa na kitu basi ajenge udugu na wafu waliyomo ndani ya makaburi.”

8 – Ishaaq bin Ibraahiym amesema:

“Kulisemwa kuambiwa al-Mughiyrah bin Shu´bah: “Ni kipi kilichobaki ambacho unastareheka nacho?” Akasema: “Kuwapa zawadi ndugu.” Akaulizwa tena: “Ni mtu gani anayeishi maisha mazuri zaidi?” Akasema: “Yule ambaye wengine wanaishi kupitia yeye.” Akaulizwa tena: “Ni mtu gani anayeishi maisha mabaya zaidi?” Akasema: “Yule ambaye hakuna yeyote anayeishi kupitia yeye.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 242-246
  • Imechapishwa: 31/08/2021