Mtoto anaweza kumswalia mzazi wake aliyekufa?


Swali: Je, kuna swalah ambayo mtoto anawaswalia wazazi wake waliofariki?

Jibu: Hakuna swalah ambayo watoto wanawaswalia wazazi wala mtu mwengine baada ya kufa. Kilichowekwa katika Shari´ah ni kuwaombea du´aa, msamaha, kuwatolea swadaqah na kuwafanyia hajj na ´umrah. Kuhusu swalah haikuwekwa katika Shari´ah kwa yeyote kumswalia yeyote. Kilichowekwa katika Shari´ah ni kumswalia maiti wa kiislamu kabla ya kuzikwa. Ambaye hakuwahi kumswalia kabla ya kuzikwa basi imewekwa katika Shari´ah kumswalia baada ya kuzikwa akiwa muda hauzidi mwezi mmoja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliswalia kaburi la Sa´d bin ´Ubaadah baada ya kuwa limeshafanya mwezi mmoja. Vivyo hivyo sunna ya Twawaaf ambayo ni Rak´ah mbili baada ya Twawaaf zimewekwa katika Shari´ah kwa yule ambaye ametufu. Kadhalika mwenye kumuhijia na mwenye kumfanyia mwengine ´umrah imewekwa katika Shari´ah akimfanyia Twawaaf yule aliyemkalia niaba basi aswali Rak´ah mbili zinazofuatia hiyo Twawaaf.

Msingi wa yote haya ni kwamba ´ibaadah ni kwa kukomeka. Hakuna kilicho katika Shari´ah isipokuwa kile kilichothibiti dalili ndani ya Qur-aan na Sunnah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (08/352)
  • Imechapishwa: 25/06/2021