Salafiyyuun wanajishughulisha na elimu peke yake na si ´ibaadah

Swali: Kisha akamlizia ukosoaji wake kwa kuwakosoa Salafiyyuun na kusema:

“Kuna kundi la tatu ambalo limetilia umuhimu Uislamu wa elimu peke yake. Shughuli yao kubwa ni kuzisahihisha Hadiyth na kuzidhoofisha na kuwafanya watu kuwa huru kutokamana na Hadiyth dhaifu na mapokezi yaliyozuliwa. Aidha ni nyonge katika ´ibaadah na wamepumbaa juu ya hali halisi ya ummah na vitimbi vya maadui dhidi yake.”

Je, Salafiyyah na Salafiyyuun Uislamu wao ni huu wa kielimu ambao ameukosoa mwandishi huyu? Je, Uislamu wao umefupika juu ya sehemu hii ya dini na kwamba kufanya hivo ni katika mirathi ya nyumati zilizotangulia? Je, ni kweli kwamba wamepumbaa juu ya hali halisi ya ummah na vitimbi vya maadui dhidi yake na kwamba ni wanyonge upande wa ´ibaadah? Tunataraji unaweza kutuwekea wazi mambo haya.

Jibu: Himdi zote ni stahiki ya Allaah. Tunamhimidi Yeye, tunamtaka msaada na msamaha. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpotosha, na yule aliyepotoshwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake:

Amma ba´d:

Simtambui mtu maalum ambaye anazungumza namna hii au anayeelekeza tuhuma kama hizi dhidi ya Salafiyyuun. Kama mtu huyo kweli yupo, basi hapana shaka kwamba ni lazima awe mmoja kati yaa watu wawili:

Ima ni mjinga juu ya ulinganizi wa Salafiyyah na kundi lake liliopo katika nchi zote za kiislamu ulimwenguni. Daima ni wenye kutangaza kwamba ni lazima kurejea katika Qur-aan na Sunnah kwa mujibu wa mfumo wa Salaf. Wote, pasi na kujali ni wapi walipo, nchi zao na ni watu gani, wanaita ulinganizi wa haki mmoja na si wenye kutofautiana kabisa tofauti na yalivyo makundi mengine ambayo pengine fikira na ´Aqiydah zao zikatofautiana ilihali ni wenye kujinasibisha kwenye pote au kundi moja.

Kama kweli mtu huyu yupo, basi kama nilivyotangulia kusema ni mmoja kati ya watu wawili. Ima akawa ni mjinga juu yale wanayotangaza kila siku kwamba wanafata Qur-aan na Sunnah kwa mujibu wa Salaf. Au anajifanya ni mjinga juu ya hali halisi hii ilihali yeye mwenyewe anazungumza juu ya ulazima wa kuwa na utambuzi kuhusu mambo ya kisasa.

Hali halisi ya Salafiyyah ni kwamba wanalingania kufata yale yote yaliyomo ndani ya Qur-aan na Sunnah katika ´Aqiydah na hukumu pasi na kujali zinahusu ´ibaadah, biashara, mwenendo na mengine. Kwa ajili hiyo miongoni mwa ujinga wa kupindukia na kiburi cha hatari sana ni kule kuwanasibishia watu hawa wanaolingania kufuata Qur-aan na Sunnah kwa mujibu wa uelewa wa Salaf kinyume kabisa na kile wanacholingania.

Kuhusu kuwatuhumu kwamba ni wanyonge katika ´ibaadah, ukweli wa mambo ni kwamba hizi ni tuhuma ambazo kila mtu ambaye hamchi Allaah (´Azza wa Jall) na wala hana fungu hapa duniani na huko Aakhirah anaweza kuja nazo. Sina ninachoweza kusema juu ya tuhuma hizi zaidi ya kwamba ni uwongo mkubwa. Nilikuwa napenda kujua mfano wa tuhuma hizi zimechapishwa ndani ya kitabu au zimerekodiwa kwenye kaseti ili tuweze kuzirejea na kuzisoma kwa ajili ya kuweza kuzitambua kama alivozizungumza mwenye nazo na pia ili tuweze kuziraddi vilivyo.

Mimi hivi sasa pindi ninapozungumzia Salafiyyah, basi mimi nazungumzia ulinganizi yenyewe kama yenyewe. Ama kusema kwamba yuko mtu mmoja mmoja kati yao ambaye anaguswa na sifa hizi pungufu, hili ni jambo ambalo linaweza kupingwa na kundi lolote.

Tunajua kuwa ulinganizi ambao alikuja nao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa msafi na akawalea nao Maswahabah zake. Pamoja na hivyo walikuweko Maswahabah ambao hawakutendea kazi baadhi ya nyanja za ulinganizi huu. Hiyo haina maana kwamba hawakuwa na ulinganizi huu kwa ujumla wake. Mtu ni mwenye kukosea. Pindi baadhi ya watu wanapokosea na wakaenda kinyume na ulinganizi katika nyanja fulani, haijuzu kwa mtu ambaye anamcha Allaah akapindua uhakika wa ulinganizi kwa sababu eti tu wapo baadhi ya watu wanaoenda kinyume na ulinganizi huo katika baadhi ya nyanja zake.

Mtu huyu akifanya hivo na akaonelea kuwa wote ni wenye kasoro kwenye ´ibaadah kwa sababu ya upindaji wa baadhi ya watu, basi nafikiri kwamba kila ulinganizi – na tufanye pia hiyo ambayo inalinganiwa na mtu huyo – una watu wengi mfano hao ambao wanaenda kinyume na yale ambayo yanalinganiwa na mtu huyo kutokamana na ule ulinganizi wenye kuenea ambao anahimiza. Akiwa ni mwenye kutangaza kwamba ulinganizi wake ni wenye kuenea kila nyanja ya kiislamu iliotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah, basi si sahihi kwetu kusema kwamba mambo sivyo juu ya nafsi yake mwenyewe au mwengine kwamba amefanya mapungufu kwa kile kitu anachowalingania watu kwacho. Kufanya hivo itakuwa sio uadilifu. Hii itakuwa ndio dhuluma yenyewe. Hapa tunasema yale yaliyosemwa na Mola wetu (Tabaarak wa Ta´ala):

وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ

“Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na kumcha Allaah.”[1]

[1] 05:08

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (611)
  • Imechapishwa: 24/06/2021