Kumdiriki imamu katikati kwenye swalah ya jeneza


Swali: Ni ipi hukumu na nifanye nini nikijiunga na imamu katika swalah ya jeneza na tayari ameshapiga baadhi ya Takbiyr?

Jibu: Swalah ya jeneza ni faradhi kwa baadhi ya watu ambapo wenye kuiswalia wanalipwa thawabu za kutekeleza kitendo cha wajibu. Mtu akiingia na imamu tayari ameshapiga baadhi ya Takbiyr, ajiunge nae na aombee du´aa kuanzia pale katika ile Takbiyr aliyomdiriki imamu. Kwa mfano lau atajiunga akamkuta imamu yuko katika Takbiyr ya tatu – ambayo ndio anayoombewa maiti – ajiunge nae na amuombee maiti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yale mtayowahi swalini, na yale yatayokupiteni kamilisheni.”

Kisha imamu akitoa Tasliym ya swalah ya jeneza, maamum akamilishe yale yaliyompita ikiwa jeneza litabaki mpaka ayakamilishe. Jeneza likinyanyuliwa kabla hajakamilisha, basi ana haki aidha ya kutoa Tasliym au kupiga Takbiyr zilizompita na halafu baada ya hapo ndio atoe Tasliym. Hivi ndivyo walivyosema wanachuoni juu ya masuala haya.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (01)
  • Imechapishwa: 09/09/2020